16 August 2012
Dkt. Kigoda awataka wawekezaji
Korea kuwekeza nchini Tanzania
Na Mwandishi Maalumu, Seoul Korea Kusini
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini Korea kuja nchini Tanzania ili kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Sekta hizo ni pamoja na ile ya utalii ambayo ina fursa nyingi za uwekezaji kama malazi, usafirishaji watalii na utalii wa majini.
Dkt. Kigoda aliyasema hayo hivi karibuni jijini Seoul, nchini Korea wakati wa mkutano wa kibiashara kati ya wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 100 nchini hapa.
Wawekezaji hao wanatoka katika sekta mbalimbali ambapo mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi pamoja na wanachama wa Jumuia ya Watanzania waishio nchini Korea.
Akizungumzia suala la utalii barani Afrika, Dkt. Kigoda aliwaeleza wawekezaji hao kuwa Tanzania ni eneo bora la utalii lenye vivutio vizuri ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika
Alitumia fursa hiyo kumpongeza mwanamuziki maarufu nchini hapa mwenye mashabiki wengi aliyejulikana kwa jina moja la Choy kwa kazi nzuri ya kuutangaza Mlima Kilimanjaro nchini hapa kupitia sanaa ya muziki.
“Tanzania ina utajiri wa vivutio vya utalii, Mlima Kilimanjaro uko Tanzania si nchi nyingine yeyote, namshukuru sana mwanamuziki Choy kwa kuutangaza mlima huu,” alisema Dkt. Kigoda.
Mbali ya mlima huo ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika, vivutio vingine ni Bonde la Ngorongoro, ambalo ni kati ya maajabu nane ya dunia, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Visiwa vya Zanzibar ambavyo ni maarufu kwa utalii wa fukwe na maeneo ya kihistoria.
Nje ya mkutano huo kulikuwa na maonesho madogo ya utalii wa Tanzania ambapo wawekezaji hao walipatiwa vielelezo vya utalii na maelezo yaliyokuwa yakitolewa na maafisa kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA).
Mkutano huo uliandaliwa na Mamlaka ya Biashara nchini (TANTRADE), ambayo ilishirikiana na Chama cha Watanzania waishio nchini hapa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment