24 August 2012
Mwakyembe aibua ufisadi bandarini *Mkurugenzi Mkuu asimamishwa kazi na wengine watatu *Kisa utendaji mbovu, wizi, rushwa, uchunguzi waendelea
Na Agnes Mwaijega
WAZIRI wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), kuwasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Bw. Ephrahim Mgawe na wasaidizi wake watatu kwa tuhuma za wizi, rushwa na utendaji mbovu.
Pia Dkt. Mwakyembe ameiagiza bodi hiyo kuwasimamisha kazi Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Jason Rugaihuruza, Meneja wa Mafuta ya Ndege Kurasini, Meneja wa Jet pamoja na Meneja wa Oil Terminal.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dkt. Mwakyembe alisema, wateja wa ndani na nje ya nchi wamepoteza imani na mamlaka hiyo kwa sababu ya kukithiri vitendo viovu katika bandari hiyo pamoja na utendaji mbovu.
Alisema kuanzia sasa, Mhadisi Madeni Kipange, kutoka Wizara ya Ujenzi atakaimu nafasi ya Bw. Mgawe na kuongeza kuwa, viongozi hao wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi huru na haki juu ya tuhuma ambazo zinawakabili.
“Wateja wengi wa ndani na nje wameacha kutumia bandari hii kutokana na hofu ya upotevu wa mizigo yao, kumekuwa na tabia ya wizi na upotevu mkubwa wa mafuta katika meli zinaoingia nchini,” alisema.
Dkt. Mwakyembe aliiagiza bodi hiyo kuhakikisha inarejesha kifaa cha kupimia mafuta (flow meter), yanayoingia bandarini ili kudhibiti wizi huo na kutambua kiasi cha mafuta kinachoingizwa nchini.
Alisema Wizara hiyo imebaini wizi wa makontena yaliyobeba mizigo ya wateja ambao hivi sasa wamekosa imani na TPA.
“Jana (juzi) kuna kontena moja la vitenge la mama mmoja limepotea, mwenyewe alikuwa akilia na hajui limepoteaje, kwa mamlaka niliyopewa, itakuwa makosa makubwa kwa uongozi wa Wizara kuacha hali hii iendelee kwani tayari tumepoteza wateja wengi wa ndani na nje ya nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa, kutokana na udhaifu mkubwa wa kiutendaji uliopo katika mamlaka hiyo, Wizara imeunda Kamati Maalumu ya watu saba ambayo itafanya uchunguzi wa kina kwa wa wiki mbili ili kubaini wahusika wakuu wa matatizo yanayotokea.
“Tumeamua kutafuta mtu kutoka nje ya Wizara na TPA ili aweze kufanya kazi hii vizuri ndio maana nimemteua Mhandisi Madeni Kipande, kutoka Wizara ya Ujenzi, akaimu nafasi ya Bw. Mgawe,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliagiza kufikia Septemba mosi mwaka huu, malipo yote ya TPA yafanyike benki au kwa kutumia njia nyingine za kisasa badala ya kuendelea kufanyika dirishani.
Wakati huo huo, Dkt. Mwakyembe ameiagiza bodi hiyo kuisimamisha Kampuni ya Singirimo, iliyokuwa imepewa zabuni ya kuchukua mafuta machafu katika bandari hiyo ili kupisha uchunguzi unaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema kampuni hiyo imekuwa ikiiba mafuta safi na kudai ni machafu hivyo kusaababisha hasara kubwa.
“Kampuni hii imefanya kazi kwa muda wa miaka mitano na kusababisha hasara kubwa hivyo naomba kuanzia sasa isimamishwe na kama itawezekana, kazi hii ipewe kampuni nyingine ambayo ilishinda zabuni,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Pamoja sana Mzee Wetu.. Umefanya jambo la maana. Kwanza waliona bandari kama ya babao kiasi wafanye wanavyotaka. Chezea wewe..
ReplyDelete