24 August 2012

Muhongo: Tutaendelea kusafirisha mchanga wa dhahabu nje ya nchi


Na Raphael Okello, Bunda

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema Serikali itaendelea kusafirisha mchanga ya madini nje ya nchi ili ukafanyiwe uchunguzi kutokana na ukosefu wa maabara zenye uwezo wa kubaini aina mbalimbali za madini nchini.


Alisema kusafirishwa kwa mchanga huo, si wizi bali hali hiyo inachangiwa na ukosefu wa vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kuchambua aina tofauti za madini.

Prof. Muhongo aliyasema hayo juzi wakati akihitimisha ziara yake katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara waakati akijibu swali la mkazi wa Kijiji cha Mwibara, Bw. Qudra Maalim.

Bw. Maalim alitaka kujua sababu ya mchanga ya dhahabu kutoka migodi mbalimbali kusafirishwa kwa ndege kwenda nchi za nje ambapo Prof. Muhongo alisisitiza kuwa, si Tanzania pekee inayofanywa bali nchi nyingi zinasafirisha mchanga huo.

“Serikali itaendelea kusafirisha mchanga huu wakati ikiendelea kutafuta njia mbadala, katika migodi mingi ya dhahabu yapo madini mengine kama shaba, fedha na kopa.

“Madini haya unaweza kuyakuta katika michanga ya dhahabu na suluhisho pekee la kutopeleka michanga nje ni kujengwa maabara za kisasa zenye uwezo wa kufanya uchambuzi,” alisema.

Aliongeza kuwa, maabara zilizopo zina uwezo wa kubainisha dhahabu katika miamba ya madini kwa asilimilia 40 hivyo ili kufiki asilimia 100 ya uchambuzi huo, asilimia 60 ya michanga itokanayo na miamba hupelekwa nje kuchambuliwa kwenye maabara za kisasa.

Alizitaja baadhi ya nchi zenye maabara za kisasa kuwa ni Ujerumani na Marekani ambapo pamoja na kufanya kazi ya madini nchini, hajawahi kutumia maabara kuchunguza miamba ya madini kwa sababu uwezo wake ni mdogo.

“Niseme ukweli kwamba, mimi nilisoma katika nchi zenye maabara ya hali za juu kama Ujerumani, pamoja na kufanya shughuli za nishati na madini, sijawahi kutumia vipimo vya mahabara zilizopo nchini kwetu, huu ndio ukweli,” alisema Prof. Muhongo.

Alisema ili kuondoka na hali hiyo, Watanzania wasipoteze muda mwingi kulumbana kwa masuala ya kizushi bali wachape kazi na kutafuta ubunifu za kukimbizana na nchi zinazotuzunguka.

Aliwabeza wananchi wanaotaka Tanzania ichimbe madini yenyewe na kudai kuwa, teknolojia yetu ni ndogo na wataalamu wachache waliopo hawana budi kushirikiana na wenzao kutoka nje.

Hata hivyo, Prof. Muhongo alisema Wizara yake imeweka mikakati ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuingia mikataba na kampuni zinazochimba madini.

Akiwazungumzia wachimbaji wadogo, Prof. Muhongo alisema mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imetenga sh. bilioni 8.9  ili kuboresha utendaji kazi wao na kuwataka waunde ushirika wao wa Akiba na Mikopo SACCOS au kampuni katika maeneo yao ili Serikali iweze kuwawezesha.

Aliwataka wananchi vijijini kuweka mikakati ya kuanza kutumia umeme kuanzia Januari 2013 kutokana na gharama zake kushushwa ili waweze kupunguza ukali ya maisha.

“Niliamua kulishinikiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lishushe bei ya umeme ili wananchi wengi waapate nishati hii na kubadili mfumo wa utendaji wa shirika kwa kuiboresha.

“Mkakati wa Serikali ifikapo 2025, idadi ya watumiaji umeme ifikie asilimia 50 ya Watanzania wote, tunahitaji uzalishaji wa megawati 4,000, hadi sasa tunazalisha 420,” alisema.

Alisema kwa kuanzia wataanza kutumia umeme wa makaa ya mawe na gesi ambapo tayari dola za Merakani bilioni 1.255, zimepatikana kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Bahari ya Hindi mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam.

Alisema umeme huo utazalisha bidhaa mbalimbali za kilimo, viwanda na mawasiliano hivyo kuepuka uharibifu wa mazingira kutokana na matumizi ya kuni.


2 comments:

  1. Laah, hawa watu wanatunyoya mpaka mchanga wa nchi yetu wanahamisha. Kama nia yao ni madini wakishayapata kwa nini hawarudishi mchanga wa nchi yetu japo tujaze mashimo wanayotuachia? Kuna taarifa huko kwao wanajaza bahari na mchanga wetu na kupata ardhi. Waache geresha tupate hizo mashine na utaalam tumalize kila kitu hapa na sio kuhamisha nchi yetu kwao.

    ReplyDelete
  2. Tanzania inashindwa nini kuwa na maabara ya kisasa? uwezo wa kufanya hivyo upo, pesa nyingi na mali nyingi za Tanzania zinapotea kwa sababu zisizokuwa na msingi. Hawa viongozi wetu hawa-wajibiki kwa sababu wanaendelea kupata ten percent commission kutokana na hiyo mikataba isiyoeleweka kwa watanzania. Watanzania tuamke na tuunde nguvu za pamoja kuikomboa nchi yetu kutoka mikononi mwa mafisadi.

    ReplyDelete