24 August 2012

Hakimu akwamisha kesi ya kusafirisha binadamu Yemen



Na Grace Ndossa

KESI inayohusu biashara haramu ya kusafirisha binadamu nchini Yemen inayomkabili mfanyabiashara mkazi wa Arusha, Bw. Salim Ally, imeahirishwa kwa sababu hakimu anayeisikiliza Bw. IIvin Mgeta, kupata udhuru.


Wakili wa Serikali Bw. Hamidu Mwanga, aliyasema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Faisal Kahamba, wakati imekuja ili kuendelea na ushahidi mahakamani hapo.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Kahamba aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 4-5 mwaka huu, ambapo mashahidi upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi wao.

Bw. Ally anatuhumiwa kuwasafirisha Bw. Abduswamad Zakaria, Bw. Hamidu Biabato, Bw. Raufu Biabato na Bw. Sadick Almas, kutoka Tanzania kwenda nchini humo.

Inadaiwa kuwa, walalamikaji walisafirishwa na mshtakiwa ili kwenda kumjengea nyumba ya ghorofa tatu baada ya kuoneshwa michoro ya jengo na kusaini mkataba wa ujenzi.

Baada ya walalamikaji kufika nchini humo, mshtakiwa aliwapokonya hati zao za kusafiria na kuwalazimisha wajenge kujenga jengo hilo ili aweze kuwapa malazi na chakula.

Kutokana na hali hiyo, walalamikaji walilazimika kujenga jengo hilo kuanzia Septemba 2010 hadi Julai 2011, bila kupewa malipo yoyote na baada ya kuona wanaendelea kuteseka, mmoja wao alifanikiwa kuwasiliana na ndugu yake aliyepo nchini.

Ndugu huyo ni Kanali Lubinga wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambaye aliwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambao nao kuwasiliana na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini Juni 14,2011.

Juni 22,2011, Wizara hiyo iliwasiliana na Shirika la IMO ambalo lilifanikiwa kujua mahali ambapo walalamikaji walikuwa wakifanya kazi na kuwarudisha nchini kwa matakwa ya mshtakiwa Julai 23,2011 na baadae taarifa za tukio hilo kufikishwa polisi.


No comments:

Post a Comment