07 August 2012

Mshambuliaji Stella Abdijan kutua Simba *Rage aitaka Yanga ilipe mil. 60/- *Yabanwa 1-1 na Jamhuri Super 8



Na Suleiman Mbuguni

UONGOZI wa Simba umesema unatarajia kumleta mshambuliaji wa kati kutoka timu ya Stella Abdijan na pia anachezea timu ya Taifa ya Ivory Coast, Sihaone Abdulaziz ambaye anatarajia kutua nchini Agosti 9, mwaka huu kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo.

Akizungumza katika Mkutano wa Kawaida wa mwaka uliofanyika katika Ukumbi wa Polisi Mess,Osterbay, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo Aden Rage, alisema mchezaji huyo anakuja kwa mkataba maalumu wa mwaka mmoja au miwili ambapo baada ya hapo atakwenda nchini Hispania kucheza soka la kulipwa.

"Mchezaji huyu ambaye anacheza namba tisa anakuja kwa mkataba maalumu na timu yake ya Stella Abdijan, tunaingia nayo mkataba ambapo atauzwa akitokea Simba hivyo nasi tutafaidika na mchezaji huyo.

"Sisi ni wasikivu na ndiyo maana mlivyotuambia turekebuishe pale kati tuliwasikia na pia mlivyotuambia turekebishe pale mbele tumewasikia,hivyo tunawaomba na nyinyi mtusikilize," alisema Rage.

Alisema wana uhakika timu yao kwa sasa ni nzuri kwani wamefanya marekebisho kwa kumsajili beki wa APR, Mbui Twite ambaye kwa sasa yupo kwao Kinshasa, Congo DRC kwa mapumziko lakini wiki ijayo atakuwepo nchini kujiunga na wenzake.

Rage alisema pia wamemsajili, Mrisho Ngassa kwa lengo la kuziba pengo lililoonekana katika sehemu ya ushambuliaji hivyo amewataka wanachamaa kuvuta subira kwani timu yao wataiona katika tamasha la Simba Day, litakalofanyika keshokutwa ambapo watacheza na Nairobi City ya Kenya.

Akizungumzia suala la Emmanuel Okwi, alisema kwamba mchezaji huyo amefanya vizuri katika majaribio yake nchini Austria isipokuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria, hivyo kama akipona atapata mkataba wa kulipwa euro 30,000 kwa mwezi sawa na sh. milioni 60.

"Tunachotakiwa ni kumuombea Okwi apone ili arudi tena Austria kwa ajili ya kujiunga na timu yake mpya, kwani kama atafanikiwa tutafaidia na euoro 600,000 ambazo zitasaidia kujenga uwanja wetu uliopo Bunju ambao tayari tumelipa ardhi sh. milioni 50 na tunadaiwa sh. milioni 30.

"Tunajua kuna wengine wanataka ashindwe ili asiende kucheza mpira wa kulipwa, lakini tunataka mmuombee ili apone na aweze kwenda katika timu hiyo," alisema.

Mwenyekiti huyo pia alisema kwamba wanatarajia kumpeleka Austria mchezaji wa timu yao ya vijana ya wenye umri wa miaka 20, Ramadhan Singano 'Messi' kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.

Alisema tayari ameshasaini kila kitu kinachohusu kwenda kwake nchini humo, hivyo anatarajia atakaporudi kutoka Nigeria ambapo amekwenda na timu ya Taifa ya vijana (Ngorongoro Heroes), ataunganisha moja kwa moja kwenda Austria.

Rage alisema wameamua kuwapeleka wachezaji wao nchini Austria kwa kuwa wamejenga urafiki na watu wa huko.

Pia alisema kuna wachezaji watano wa timu ya vijana ambao walikuwa nje kwa majaribio na kama mambo yatakwenda vizuri kila mmoja atauzwa kwa uero 500,000 ambazo fedha hizo zitatumika kuzipeleka timu za vijana katika nchi za Ulaya kucheza michuano ya vijana ili kuwajenga na kuwatafutia timu za kucheza.

Katika hatua nyingine, Rage alisema wanawapa Yanga hadi Ijumaa wawe wamepeleka sh. milioni 60 kwa ajili ya beki, Kelvin Yondani kwa kuwa mchezaji huyo ni mali yao na wana ushahidi wa mkanda wa video wakati akisaini upya, vinginevyo watahakikisha mchezaji huyo hachezi Yanga kwa kuwa hivi sasa wanafanya mipango ya kulipeleka suala hilo Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Naye Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambao ndiyo wadhamini wa klabu hiyo, George Kavishe alisema wanaona fahari kufanya kazi na viongozi wa Simba kwa kuwa wamekuwa wakishirikiana kwa karibu hasa katika masuala ya mapato na matumizi.

Alisema ahadi ya basi la kisasa ipo palepale, isipokuwa ratiba ya kwamba ingekabidhiwa keshokutwa imeshindikana kwa kuwa basi hilo ni aina ya Coach Athletics ambalo ni maalumu na linahitaji baadhi ya vitu vya ziada kuwemo kama sehemu ya mizigo nafasi ya kuwawezesha wachezaji kukaa vizuri wakati wa safari, hivyo badala ya kuja siku hiyo kwa sasa siku zitaongezeka.

Wakati huohuo, viongozi na wanachama wa Simba jana walichanga zaidi ya sh. milioni 30 za papo kwa hapo kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa uwanja wa michezo wa klabu hiyo uliopo Bunju, Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu, Speciroza Joseph anaripoti kutoka Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwamba mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Zanzibar katika mechi za michuano ya Super 8.

Jamhuri ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika 47 lililofungwa na Bakari Hamis na Simba ilizawazisha dakika ya 84 kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Shomari Kapombe.Simba ilichezesha wachezaji wengi wa timu yao ya vijana.

No comments:

Post a Comment