07 August 2012

Manji apitisha 'fagio la chuma' Yanga *Mkuchika aongezwa Bondi ya Udhamini



Na Amina Athumani

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amezivunja kamati zote za Yanga isipokuwa Kamati ya Uchaguzi ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa klabu.

Maamuzi hayo yamefanywa jana na Mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na kamati nzima ya Utendaji ya Yanga katika makao makuu ya klabu hiyo, mara baada ya kusimikwa na kupatiwa kiapo cha kuitumikia klabu hiyo.


Viongozi waliosimikwa na kula kiapo ni Manji, Makamu Mwenyekiti, Clementi Sanga na Wajumbe Aron Nyanda, George Manyama na Mussa Katabaro ambao waliapishwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Jabir Katundu mbele ya mlezi wa timu hiyo,Mama Fatma Karume.

Bara baada ya kula kiapo, Manji akiiongoza Kamati ya Utendaji katika kikao kilichodumu kwa muda wa saa 2:30 ambapo mambo mbalimbali walikubaliana ikiwemo kuzivunja kamati zote ndogondogo na kuundwa kamati mpya.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Manji alisema kamati hiyo imeamua kuvunja kamati zote ili kupunguza matumizi ambapo kamati ya Utendaji itakuwa ni mwenyekiti wa kamati zote mpya zitakazoundwa.

Pamoja na kuvunjwa kwa kamati hizo, pia kamati ya Utendaji imeteuwa wajumbe watatu watakaoongeza idadi ya wajumbe na kufikia nane ambapo wajumbe walioteuliwa jana ni Isac Chanji na Mohamed Nyengi huku mjumbe mmoja bado akiendelea kutafutwa.

Pia kamati imewatangaza na kuwaongeza kwenye Bodi ya Udhamini, George Mkuchika ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora), Seif Ahmed na Amir Mpungwe ambapo kutafanyika mkutano wa kuweza kuwathibitisha katika bodi hiyo ambayo kwa sasa inaongozwa na Mama Fatma Karume na Francis Kifukwe.

Pamoja na uteuzi huo Manji pia, ameainisha majukumu mbalimbali yatakayokuwa chini ya bodi hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa akaunti na mali za klabu, madeni ya klabu na kuangalia mikataba yote ikiwemo iliyoingia klabuni humo na kampuni zake.

Alisema bodi hiyo pia ndiyo itakayokuwa ikisimamia mikataba yote itakayoingia klabuni pamoja na kukagua mahesabu ambapo pia ndiyo itakayoteuwa mwanasheria wa klabu.

Mwenyekiti huyo alisema mikutano yote ya klabu itakuwa ikifanyika makao makuu ya klabu hiyo  na itakuwa ikifanyika kwa uwazi na kwamba kwa kuanzia mkutano wa kwanza utafanyika Jumapili ijayo na itakuwa ikifanyika kila wiki na baadaye kwa kila mwezi.

Manji pamoja na wajumbe wake waliingia madarakani Julai 15, mwaka huu mara baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizokuwa wazi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga pamoja na baadhi ya wajumbe wake.

No comments:

Post a Comment