23 August 2012

Mramba amtaja Mkapa kortini *Ni katika kesi ya kutumia madaraka vibaya *Adai ndiye aliyebariki ujio Kampuni Alex Stewart *Chenge, Cheyo, Gavana kumtetea mahakamani


Na Grace Ndossa

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Bw.Basil Mramba, anayekabiliwa na kesi ya kutumia vibaya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya sh.bilioni 11.7, ameanza utetezi wake ambapo amemtaja Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Bw.Benjamin Mkapa kuwa alibariki Kampuni ya Alex Stewart kuingia nchini.


Alisema Rais Mstaafu Mkapa alihusika kuweka baraka zake Benki Kuu ya Tanzania(BoT) kuitafuta kampuni hiyo kuja nchini kufanya ukaguzi wa mahesabu kwenye migodi iliyokuwa ikilalamikiwa

Bw.Mramba alitoa kauli hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akitoa utetezi wake mbele ya jopo la mahakimu wawili wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji John Utamwa.

Mahakimu wengine wanaosikiliza kesi hiyo ni Bw.Saul Kinemela na Bw.Sam Rumanyika wote wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Bw.Mramba alidai kuwa BoT iliagizwa na Rais Mstaafu, Bw.Mkapa kuleta kampuni hiyo nchini, hivyo yeye kama Waziri alipewa maagizo ya kuhakikisha gharama za kumlipa mshauri huyo zinapatikana.

"Nilipewa maagizo na Rais Mkapa nihakikishe fedha hizo zinapatikana ndani ya Serikali yenyewe au ndani ya BoT au zote mbili kwa ujumla," alidai Bw.Mramba.

Awali kabla ya kuanza kujitetea, Bw. Mramba na washtakiwa wenzake, Bw.Grey Mgonja aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Bw.Daniel Yona, waliambiwa na Jaji Utamwa kuwa, washtakiwa hao wana haki ya kujua haki zao.

Jaji Utamwa aliwauliza washtakiwa hao kama watakuwa na mashahidi, Bw.Mramba ambaye ndiye wa kwanza kujitetea aliiambia mahakama hiyo kuwa atakuwa na mashahidi tisa.

Bw.Mramba alisema miongoni mwa mashahidi hao ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC), Bw.John Cheyo na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Mwakilishi kutoka Kampuni ya Alex Stewart,  Government Business Asseys, Bw. Elwin Florence na Bw.Florian Msigala, ambaye ni Mtaalamu Mshauri wa Masuala ya Kodi.

Akiongozwa na wakili wake Bw.Hurbet Nyange, Bw.Mramba alidai chimbuko la kesi hiyo ni malalamiko yaliyokuwepo bungeni, miongoni mwa wananchi na vyombo vya habari, kuwa licha ya Tanzania kuwa na  migodi mingi, lakini haifaidiki nayo.

Alidai kuwa, kutokana na hoja hizo Serikali ilitakiwa kuzijibu wakati akiwa Waziri wa Fedha ambapo alitoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart ambayo ilikuwa imeletwa na Serikali kufanya kazi ya kukagua mahesabu ya migodi ili kupata majibu ya malalamiko yaliyokuwa yakitolewa.

Shahidi huyo wa kwanza alidai yeye hakuhusika katika mchakato wa kutafuta kampuni hiyo, bali Serikali iliiteua BoT kuleta mkandarasi anayefaa.

Alidai BoT ilifanya hivyo kwa kuingia mkataba na kampuni hiyo.

Bw.Mramba alidai kuwa kampuni hiyo ni moja ya Kampuni ya Alex Stewart Group ambayo makao yake makuu yapo nchini Uingereza.

Alipoulizwa na wakili wake kuwa kati ya yeye na aliyekuwa Gavana wa BoT, Marehemu Daud Balali nani aliyekuwa juu ya mwenzake, Bw.Mramba alijibu; "Kila mtu alikuwa na kazi zake."

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Bw.Mramba na wakili wake, Bw.Nyange.

Nyage: Kati ya wewe na Balali nani aliyetakiwa kumtafuta mkaguzi wa migodi hiyo?

Mramba: Ni Gavana wa BoT ambaye alikuwa ni Balali na mimi sikuhusika wala kumtafuta mshauri huyo.

Nyange: Katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapa na upande wa mashtaka, ulidai kuwa kulikuwa na kamati iliyohusika na mchakato huo, Je wewe ulikuwemo katika kamati hiyo?

Mramba: Sikuhusika wala sikumtuma mtu aniwakilishe katika kamati hiyo.

Nyange: Ulifahamu hiyo kamati ilitumia mbinu gani kuchagua kampuni hiyo?

Mramba: Nilifahamu baadaye kuwa BoT ilitangaza kwa njia ya mtandao duniani kote, ambapo walipata kampuni mbili.

Bw.Mramba alisema alifahamu baadaye kuwa Wizara yake ilimtuma Ofisa anayeitwa, Bw. Beka Soka ambaye alikuwa mwanasheria kujadili rasimu za mkataba na kampuni mbili.

Bw.Mramba alidai ofisa huyo alitumwa awe mjumbe.Baada ya majibu hayo, Wakili Nyange aliiomba mahakama akazungumze na mteja wake, lakini wakili wa Serikali Bw. Fredrick Manyanda, alisimama na kusema kuwa mshtakiwa ameshakula kiapo, hivyo hakuna nafasi ya kuzungumza na wakili wake.

Jaji alikubaliana na hoja ya wakili wa Serikali, ndipo wakili Nyange alilazimika kufanya hivyo baada ya kuona mteja wake anatoka nje ya mstari wa kile alichomuuliza.

Baadaye Bw.Mramba aliendelea kutoa ushahidi wake na kuonesha mkataba wa Kampuni ya Alex Stewart na BoT ambapo alidai kuwa mkataba huo ulisainiwa na Gavana Balali na mmoja wa wawakilishi wa kampuni hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo wanakabiliwa na mashtaka 13 ambapo kesi hiyo imeahirishwa na itaendelea kusikilizwa leo.

No comments:

Post a Comment