23 August 2012

Mchuano wa urais 2015 waibukia Hanang'


Na Mwandishi Wetu

KATIKA kile kinachohusishwa na urais wa mwaka 2015, hali ya kisiasa wilayani Hanang' mkoani Manyara imezidi kuwa tete huku kauli za wanasiasa vinara wilayani humo zikiibuka siku hadi siku.

Kwa kipindi kirefu sasa zimekuwepo taarifa za mvutano kati ya wanasiasa wawili maarufu wilayani humo, Waziri Mkuu mstaafu, Bw.Frederick Sumaye na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uchumi na Uwezeshaji, Dkt.Mary Nagu katika kusaka nafasi ya kuwakilisha wilaya hiyo kwa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.

Kutokana na mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni na CCM, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa watachaguliwa katika ngazi ya wilaya kwa lengo la kuzidi kukiimarisha zaidi chama hicho.

Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Manyara kilichofanyika Agosti 17, mwaka huu, Bw.Sumaye alikaririwa na gazeti moja akikemea vikali uwepo wa rushwa kwa viongozi na kusema kuwa mtoa rushwa hawezi kuwa kiongozi makini.

Wakati Bw.Sumaye akitoa kauli hiyo, Dkt.Nagu alikaririwa akitaka chama hicho mkoani Manyara kushikamana kinyume na hapo mkoa huo utaangukia kwa wapinzani.

Dkt.Nagu alisema hali hiyo imechangia  kukibomoa chama na kuupa upinzani nguvu na kufanya hali iwe tete.

"Mkoa ulikuwa wa CCM na kulikuwa hakuna mgawanyiko na sasa upinzani umeingia kwa nguvu sana, sisi ndiyo tunasababisha na sasa tuna wakati mugumu, tunahitaji mshikamano madhubuti kurudisha hali kama ya awali," alisema Dkt.Nagu.

Siku za hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwepo mvutano mkali kati ya wanasiasa hao na kudai kwamba mchuano huo ni moja ya hatua zinazochukuliwa mapema na wapinzani wa Bw.Sumaye ambaye amekuwa akitajwa tajwa kugombea urais mwaka 2015 kuhakikisha anadhibitiwa mapema kwenye nafasi hiyo.

Wadadisi wa masuala ya siasa za mkoani Manyara wanadai kwamba uchaguzi na mvutano wote unaoendelea wilayani Hanang' katika nafasi ya kiti cha ujumbe wa NEC ni mkakati wa makusudi kuhakikisha, Bw. Sumaye anayeonekana kuwa na nguvu kutokana na rekodi nzuri kiuchumi iliyooneshwa na serikali ya awamu ya tatu, anakwamishwa.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa mjini Hanang' wanasema kinachoendelea ni vita ya urais wa 2015. Wengi wanatafsiri kinachoendelea wilayani humo na mambo ya 2015.

"Unajua Sumaye katika awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa walifanikiwa sana kujenga uchumi na kupunguza mfumuko wa bei hadi kufikia digiti moja," alisema aliyezumgumzia hali ya kisiasa wilayani humo.

Aliongeza kuwa; "Mafanikio ya awamu ya tatu yanampa nafasi kubwa Bw.Sumaye ambaye kama unakumbuka aligombea mwaka 2005 akakosa, lakini unajua sasa watu wengi wanakumbuka mafanikio hayo na hata baadhi ya wanasiasa wanataja hadharani mafanikio hayo, kutokana na hilo wanajua kama atasimama kugombea anaweza kuwa na nafasi kubwa

1 comment:

  1. Mh! na ufisadi wake na Mkapa wake pia unakumbukwa na kutajwa tajwa hivyo hivyo na hata kumpa wakati mgumu JK kulazimika kuthubutu kuwafikisha mahakamani vigogo chini ya utawala wake! Time will tell!

    ReplyDelete