24 August 2012

Mramba akiri kutoa msamaha



Na Grace Ndossa

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Bw. Basil Mramba, amekiri kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart, iliyoletwa na Serikali ili kufanya ukaguzi wa hesabu katika migodi ya dhahabu nchini kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za mkataba.

Bw. Mramba aliyasema hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana, wakati akitoa utetezi wake kwenye kesi ya kutumia madaraka vibaya na kuisababisha Serikali hasara ya sh. bilioni 11.7.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri Nishati na Madini, Bw. Daniel Yona na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Gray Mgonja.

Ikiwa ni siku yake ya pili kupanda kizimbani, Bw. Mramba, aliiambia mahakama kuwa; “Nilitoa msahama wa kodi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za mkataba.

“Kuna kifungu cha kusamehe kodi na kuuarifu umma kuwa fulani kasemehewa kodi, kifungu hiki kilikuwepo tangu uhuru, kama Waziri angetaka kusamehe mtu kodi, kuna kifungu cha sheria ambacho humruhusu atoe msamaha kwa masilahi ya umma bila kuhojiwa na mtu,” alisema Bw. Mramba.

Aliongeza kuwa, kabla ya kutoa notisi ya kusudio la msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo, alitoa taarifa Idara ya Sheria katika Wizara ya Fedha ambapo mkataba ulipitiwa na kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiridhika kuwa mkataba huo ni sawa, unarudishwa kwa wanasheria wa Wizara, baada ya hapo anajulishwa Katibu Mkuu kuwa umeruhusiwa na mwanasheria au hapana,” alisema Bw. Mramba.

Aliongeza kuwa, baada ya mkataba huo kupewa baraka zote kwa maana ya kuruhusiwa, Katibu Mkuu anamtaarifu Waziri ambaye anatoa notisi ya kutolewa msamaha kwa kampuni husika.

Bw. Mramba alidai kuwa, utaratibu huo ndiyo aliofuata wakati wa kutoa msamaha kwa kampuni hiyo hivyo hakukuwa na ukiukwaji wowote wa sheria.

“Tulishauriwa na timu ya wataalamu iliyokaa na kuujadili mkataba huu ambayo ilisema kampuni hii ikisamehewa kodi, gharama za ukaguzi zitapungua,” alisema.

Alisema Gavana wa Benki Kuu (BoT), alishauriwa na timu iliyopatana kuhusu msamaha huo na kukubaliana ailipe malipo ya awali. “Nilimruhusu gavana atumie dola milioni moja kumlipa malipo ya awali ili Serikali ije kurejesha baadaye,” alisema.

Bw. Mramba aliongeza kuwa, kabla malipo hayo hayajafanyika, Waziri wa Nishati na Madini alimwandikia Rais barua, kuomba kibali ili airuhusu BoT na Wizara ya Fedha, kutafuta fedha ili kuilipa kampuni hiyo ianze kazi.

“Rais alikubali, nakala ya barua ilipelekwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na BoT ilipewa baraka ya kulipa fedha hizo.

“Maelekezo yote yalifanyika kama Rais alivyokuwa ameagiza na niliwahimiza wasaidizi wangu watekeleze haraka mchakato huo,” alidai, Bw. Mramba. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 12 mwaka huu kuendelea na utetezi wake.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la mahakimu wawili Bw. Saul Kinemela na Bw. Sam Rumanyika wakiongozwa na Jaji John Utamwa.

No comments:

Post a Comment