31 August 2012
Milovan: Sasa mina timu ya mashindano
Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema kwa sasa kikosi chake kipo tayari kucheza mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, kwa kuwa wachezaji wake wamezoeana na wanaelewana vizuri uwanjani.
Mechi hiyo inatarajia kuchezwa Septemba 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo tayari timu hiyo imeshacheza mechi kadhaa za kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo, pamoja na Ligi Kuu Bara.
Akizungumza kwa simu jana akiwa Arusha ambako timu hiyo imeweka kambi, Milovan alisema mechi mbili walizocheza dhidi ya Mathare ya Kenya ambayo walishinda mabao 2-1 na ile ya JKT Oljoro waliyoshinda mabao 2-1, zimemuonesha kuwa sasa wapo kimashindano.
"Kwakweli sasa hivi wachezaji wangu wanacheza kwa kuelewana vizuri mno, upo upungufu mdogo mdogo ambao naendelea kuufanyia kazi, kwani pia natarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa, ili nizidi kukitengeneza kikosi changu," alisema Milovan,
Alisema washambuliaji wake Mghana Daniel Akuffo na Mrisho Ngassa, wanamfurahisha kwani wamekuwa wakielewana vizuri hali ambayo inampa matumaini makubwa, lakini hata hivyo amedai ataendelea kukisuka kikosi hicho kwani hadi sasa hana kikosi cha kwanza.
Simba wanatarajia kucheza na timu ya Nairobi City ambayo walichezanayo Agosti 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Tamasha la Simba Day. Simba walichapwa mabao 3-1, hivyo Jumapili watarudiana Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Awali, Simba ilikuwa icheze na Coastal Union ya Tanga Jumapili Uwanja wa Taifa, lakini imeachana na mechi hiyo kwa kuwa timu hiyo itaanza kwa kucheza na watani zao Yanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment