30 August 2012
Kadinda kufanya vitu vyake New York
Na Mwandishi Wetu
MBUNIFU wa Tanzania, Martin Survivor Kadinda ‘Martin Single Button’ anatarajia kuonesha mavazi yake kesho nchini Marekani katika onesho la mavazi la New York Africa Fashion Week na Music on The Caltwalk (MOC).
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kampuni ya One Touch Solutions, Petter Mwendapole alisema Martin atakuwa huko pamoja na wabunifu wengine saba kutoka sehemu mbalimbali za Afrika.
“Martin ni mmoja wa wabunifu ambao wamechaguliwa kushiriki kwenye onesho hilo, litakaloambatana na utoaji tuzo kwa wasanii wa filamu na wanamuziki wengine wa Nigeria,” alisema.
Mbali na makoti maarufu ya Single Button, Martin ataonesha pia nguo zake mpya ziitwazo vibunduki pamoja Kivumbi Collection, ambazo kwa mara ya kwanza zilioneshwa kwenye Dar Fashion Festival.
Akizungumzia nafasi ya kushiriki onesho hilo, Kadinda alisema amefurahia kwa kuwa itampa nafasi ya kukutana na wabunifu wengine wakubwa duniani na kujifunza mambo mbalimbali katika sanaa.
“Hii ni changamoto kubwa kwangu, nitaitumia vizuri kuhakikisha naongeza ujuzi katika sekta ya ubunifu, nashukuru kwa maandalizi ambayo One Touch wamefanya kwa ajili ya kunikutanisha na watu mbalimbali nchini Marekani watakaonipa malekezo juu ya kazi yangu,” alisema.
Music on the Catwalk itafanyika Ukumbi wa Hellen Mills Event & Theater mjini New York.
MOC ni onesho la kila mwaka, ambalo limebuniwa kwa ajili ya kukuza vipaji vya wasanii wa muziki pamoja na mavazi ambapo lengo kuu ni kutangaza kazi za wasanii wa Kiafrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment