21 August 2012
Matola atoboa siri ya mafanikio
Na Speciroza Joseph
BAADA ya kutwa ubingwa wa kwanza wa Kombe la SUP8R, Kocha wa Simba B, Seleman Matola amesema jitihada, uwezo na maandalizi bora ndio sababu ya kupata mafanikio na kwamba waandaaji waboreshe mashindano hayo na kuwa ya kimataifa.
Matola aliiongoza timu hiyo na kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 4-3 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matola alisema jitihada na uwezo wa wachezaji wake ni sehemu kubwa ya kufikia mafanikio hayo ambayo ameyaita ni hatua kubwa kwa Klabu ya Simba.
"Tulianza maandalizi pindi nilipopata taarifa kuwa timu yangu itashiriki, tulijiandaa kikamilifu kwa kuwa tulijua tunaenda kupambana na timu kongwe na zenye uzoefu lakini uwezo wa wachezaji wangu ulinipatia ushindi" alisema Matola.
Aliongeza kuwa mashindano hayo hayakuwa mepesi kama watu wanavyofikiria bali yalihitaji wachezaji imara na wenye kujituma kwa kuwa kila mechi ilikuwa sawa na fainali.
Matola aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango na kupambana na timu kubwa, alisema kwao ilikuwa ni changamoto kwa kuwa Simba B ni timu pekee iliyokuwa na wachezaji wadogo.
Akizungumzia mchezo wao wa fainali, Matola alisema Mtibwa ni timu nzuri sana wametumia makosa yao kupata ushindi huo kwa kuwa anaamini kama wasingejiandaa vizuri wangeukosa ubingwa huo.
Aliongeza kuwa ili mashindano haya yapate radha zaidi ingekuwa vizuri waandaji wakaalika na timu za kutoka nje kuongeza ushindani.
Kocha huyo ambaye alikuwa mcheza wa zamani wa Simba alisema vijana hao ni zao bora kwa klabu hiyo, hivyo wakitumiwa vizuri wataisaidia timu katika Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment