28 August 2012

'Mamlaka ziingilie kati ubora wa mafuta'


Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA zinazohusika kusimamia ubora wa mafuta ya petroli, zimetakiwa kuingilia kati na kutoa majibu sahihi ili kuondoa mkanganyiko ulioibuliwa na Shirika la Viwango nchini (TBS).

Mkanganyiko huo unatokana na TBS kutangaza kuwa, mafuta yanayotumika nchini yanaruhusiwa kuchanganywa na kemikali nyingine ikiwemo ethanol.


Wiki iliyopita, TBS ilitangaza kuwa kulingana na viwango vya Tanzania, mafuta yaliyochakachuliwa kwa kuchanganywa na ethanol yanaruhusiwa kutumika nchini lakini Mei mwaka huu, shirika hilo lilipiga marufuku kuingizwa nchini mafuta hayo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya kampuni za mafuta zimeomba mamlaka husika zitoe majibu sahihi kuhusu ubora unaotakiwa ili kuondoa vitendo vya ubabaishaji.

“Hali ikiendelea kuachwa kama ilivyo, tunaweza kusimama kwa muda katika biashara hii kwa saababu TBS wanatuchanganya, Mei mwaka huu walitangaza kupiga marufuku mafuta kuchakachuliwa.

“Wiki iliyopita wametangaza kuruhusu mafuta ya petroli kuchanganywa kwa ethanol,” alihoji mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Alisema kutokana na mkanganyiko huo, wanashindwa kufanya shughuli zao na kuweka mipango ya muda mrefu hivyo ameziomba mamlaka husika kutoa msimamo ili kuondoa ubabaishaji.

Kwa muda mrefu, wafanyabiashara wa mafuta nchini wamekuwa wakilalamikia uingizwaji mafuta yaliyochakachuliwa kwa sababu yamekuwa yakiwasababishia hasara kwa kukataliwa nchi jirani.

Malalamiko hayo yalisababisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali sampuli 11 za mafuta kutoka kwenye meli zilizokuwa bandari ya Dar es Salaam.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa, kati ya sampuli hizo, 10 ziligundulika kuwa na ethanol nyingi kuliko kiwango kinachotakiwa ambapo hivi karibuni, Serikali ilitaka kupewa taarifa kamili kuhusu mchakato wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliagiza kupatiwa taarifa za kina kuhusu mfumo huo ambao baadhi ya wafanyabiashara walilalamikia kuwepo vitendo vya uchakachuaji mafuta yaliyozidishwa ethanol, hivyo kuathiri soko la ndani na nje.

Kampuni ya Augusta Energy SA, ambayo iliingiza mafuta katika kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu, imekuwa ikilalamikiwa kwa kusababisha hasara kutokana na mafuta hayo kukataliwa katika nchi jirani.

No comments:

Post a Comment