29 August 2012

Madaktari 50 kutoka India kutoa tiba Dar


Na Salim Nyomolelo

JOPO la madaktari 50 kutoka nchini India, wanatarajia kufanya maonesho ya matibabu katika ukumbi wa Diamond Jubilee Agosti 30 hadi 31, mwaka huu, kuanzia saa nne asubuhi hadi 11 jioni.


Taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana na Balozi wa India nchini, Bw. Debnath Shaw, ilisema maonesho hayo yameandaliwa na Taasisi ya Shirikisho la Biashara nchini India la Medical Tourism Destination (IMTD).

Aliwaomba watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya wajitokeze  katika maonesho hayo ili waweze kupata huduma ya matibabu ambayo itatolewa katika ukumbi huo kwa gharama za chini.

“Gharama zao zitakuwa za chini na zitamwezesha kila mwananchi mwenye matatizo ya kiafya kuzimudu na kupata huduma, India inaongoza duniani kwa kutoa huduma bora za tiba.

“Nchi yetu pia ina madaktari bingwa wanaoaminika katika utoaji huduma, mwaka huu IMTD inawaleta watoa huduma kutoka hospitali kubwa za India ambazo ni Fortis na Medanta,” alisema.

Alizitaja hospitali nyingine kuwa ni Asian Heart, Seven Hills, SRM Hospital, Vasan Eye Care na Idara ya Aayush ili kuja kuwasaidia wagonjwa waliopo nchini.

Alisema maonesho hayo pia yamelenga kutoa fursa ya wataalamu wa sekta hiyo kufahamiana wakiwemo wasomi na wadau ili kuweka jukwaa kwa mashirika na taasisi kati ya India na Tanzania waweze kushirikiana kuimarisha huduma ya afya.

Alisema watakuwepo wawakilishi kutoka hospitali na vituo vya afya vilivyopo nchini humo kikiwemo kitengo cha upasuaji, hospitali za macho, ortho care, bidhaa za afya, huduma za kiasili, utalii wa kiafya, kampuni za dawa na vituo vya physiotherapy.

“Zaidi ya nchi 30 duniani ikiwemo Marekani, Canada, Uingereza, Urusi, Uarabuni, Uganda, Tanzania, Sri Lanka na nchi za Bara la Asia, huwa wanakwenda India kupata matibabu,” alisema.

Bw. Shaw aliongeza kuwa, nchi hiyo pia inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watalii wanaokwenda kufuata matibabu.



No comments:

Post a Comment