29 August 2012
Kagasheki asikitishwa idadi ndogo ya watalii nchini
Na Mariam Mziwanda
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema idadi ndogo ya watalii wanaotembelea vivutio vingi vilivyopo nchini hairidhishi hivyo kuitaka sekta binafsi kuwa mhimili wa utalii nchini.
Balozi Kagasheki aliyasema hayo Dar es Salaam jana, katika mkutano wake na wanachama wa Umoja wa Shirikisho la Utalii nchini (TCT) na kuongeza kuwa, ipo haja ya kuangalia tatizo lililopo hasa kwa kuzingatia kuwa, Tanzania ina vivutio vingi pamoja na maajabu mengi ya dunia.
“Vivutio tunavyo, sababu ya kuingiza watalii kwa wingi tunayo na kubwa zaidi Tanzania kuna amani na utulivu, kwanini kiwango kishuke hadi kufikia 800,000 kwa sasa,” alisema.
Alisema Serikali imeona ipo haja ya kukaa na wadau wa sekta hiyo ili kubaini tatizo sambamba na kuwashirikisha wananchi kuziba mianya hewa.
Aliongeza kuwa, lengo la Wizara ni kuweka mkakati wa kuandaa midahalo ya kitaifa kila mkoa ili kusikiliza mawazo ya wananchi juu ya kuendeleza sekta hiyo.
Balozi Kagasheki alisema Sekta ya Maliasili na Utalii ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa nchi na kuondoa Taifa tegemezi hivyo ni lazima kuweka miundombinu imara.
Amewataka wadau hao kuacha kuvutana na kufarakana badala yake wafanye kazi kwa vitendo ili kuongeza takwimu za watalii wanaotembelea vivutio vilivyopo nchini ifikapo 2013.
Katika mkutano huo, wajumbe walipata fursa ya kujadili sera na sheria ya utalii nchini ili kuondoa kero zilizopo na kuhimiza vyombo vya habari kutangaza sekta hiyo ili kukuza soko lake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment