07 August 2012
Kikwama kwa utekelezaji miradi ya maendeleo athari kwa CCM- 2015
Na Suleiman Abeid
MOJA ya mambo ambayo Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010 hadi 2015 yaliwekwa bayana ni suala kilimo.
Ndani ya ilani hiyo imeelezwa wazi kuwa kilimo ndiyo msingi wa uchumi wa kisasa na njia sahihi ya kuutokomeza umaskini.
Katika Ibara ya 31 ya Ilani hiyo, inaelezwa kuwa, nanukuu; “…Chama Cha Mapinduzi kinaamini kwa dhati kwamba iwapo kilimo cha kisasa kinachotumia kanuni na zana bora za kilimo ndiyo ufunguo wa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu,”
“Kilimo cha kisasa kina uwezo wa kutoa mazao mengi zaidi kutoka kila ekari iliyolimwa. Kwa nchi yetu, ziada hiyo ya mazao ina faida kubwa zifuatazo; (a) Kuipatia kila familia, kijiji na Taifa chakula cha kutosha ili kukomesha njaa,”
“(b) Kulipatia Taifa mavuno mengi ya kuuza ili kupata fedha za kigeni kwa ajili ya maendeleo ya nchi, (c) Ziada ya mazao huunda mazingira muafaka ya kuanzishwa viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani,”
“(d) Familia yenye ziada ya mazao huutokomeza umaskini kwa kuuza ziada hiyo kwenye soko na kupata fedha za kujiletea maendeleo,” mwisho wa kunukuu. Vifungu hivi ni moja vifungu vilivyotumiwa na wagombea wa CCM katika kipindi cha kampeni wakiomba wananchi wawachague ili waweze kutekeleza ahadi hizo.
Kutokana na hali hiyo kuna kila sababu ya Chama Cha Mapinduzi hivi sasa kusimama kidete kuhakikisha kinaisimamia kikamilifu serikali yake kuona kwamba inatekeleza vyema miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa kwa wananchi.
Kwa kadri ya hali ya mambo inavyokwenda ipo hatari ya baadhi ya miradi mingi ya maendeleo hasa katika kipindi hiki cha mwaka 2011/2012 na 2012/2013 ikashindwa kutekelezwa kama ilivyokuwa inatarajiwa kutokana na serikali kushindwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika kipindi cha mwaka 2011/2012 serikali haikuweza kutoa fedha katika halmashauri za wilaya ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kumsaidia mkulima kwa kumpatia mafunzo yatakayomwezesha kulima kilimo cha kisasa.
Halmashauri nyingi hivi sasa zinatekeleza miradi yake ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani baada ya kushindikana kupatikana kwa ruzuku iliyokuwa ikitolewa na serikali kama fidia ya vyanzo vya mapato vilivyofutwa na serikali ambapo kiasi cha fedha hizo kilichopelekwa katika halmashauri hizo kwa kipindi hicho hakikuzidi asilimia 35.
Kukosekana kwa fedha hiyo ya ruzuku iliyokuwa ikiunganishwa na fedha nyingine zilizokusanywa katika halmashauri za wilaya ni wazi kutachangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo sambamba na uanzishwaji wa miradi mipya.
Hali hii inaweza kuiathiri vibaya CCM katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015 na ule wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2014 ambapo ni miaka miwili tu iliyosalia kuelekea uchaguzi huo na ikiwa ni miaka mitatu nchi yetu itafanya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni wazi kwamba iwapo ahadi zilizoahidiwa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hazitakuwa zimetekelezwa kama ilivyokuwa imeahidiwa na wagombea mbalimbali wa CCM hadi ifikapo mwaka 2015, wagombea wake kwa mwaka huo watakosa la kuwaeleza wananchi.
Kwa mfano katika ilani hiyo Ibara ya 33 nanukuu; “…Katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya utekelezaji wa Ilani ya 2010 – 2015, Chama kitazielekeza serikali kutekeleza kwa ukamilifu malengo ya Mpango wa Maendeleo ya sekta ya Kilimo (ASDP) pamoja na kauli mbiu ya kilimo kwanza.”
Kifungu (d) kinasema; “Kuongeza upatikanaji na utumiaji wa pembejeo za kilimo, hususan mbolea, mbegu na miche bora na kuweka mfumo utakaohakikisha upatikanaji wa pembejeo hizo kwa wakulima,”
“(e) Kuongeza upatikanaji na matumizi ya zana za kilimo kwa kuishirikisha sekta binafsi, kuhamasisha na kuwezesha vikundi vya wakulima, hususan vijana kupata mikopo ya pembejeo na zana za kilimo kutoka kwenye mfuko wa pembejeo,” mwisho wa kunukuu.
Hizi ni ahadi ambazo CCM inapaswa kuhakikisha kwamba zinatekelezwa kwa wakulima nchini na ielewe kwamba zisipotekelezwa wagombea wake itakaowasimamisha kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya serikali watakuwa na wakati mgumu wa maswali kutoka kwa wapiga kura.
Baadhi ya sababu zinazoonekana kuchangia kukwama kwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ni kutokuwepo ufuatialiaji na usimamizi makini katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Lakini pia lipo tatizo kubwa la baadhi ya viongozi waliokabidhiwa jukumu la kuongoza serikali kushindwa kuwatumikia kikamilifu watanzania hususan wakulima ambao kadri siku zinavyokwenda hali zao za kimaisha zimekuwa zikiendelea kuporomoka kutokana na mazao yao kutopata bei nzuri katika soko.
Wakulima wa zao la pamba ni moja ya waathirika wakubwa kutokana na waliokabidhiwa jukumu la kusimamia kilimo nchini kushindwa kuwasaidia kikamilifu ikiwemo Bodi ya Pamba (TCB) ambayo ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha wakulima hao wanapata pembejeo za kilimo zilizo bora.
Mbali ya upatikanaji wa pembejeo bora, pia bodi hiyo ina jukumu la kuhakikisha inamsaidia mkulima kuweza kupata soko zuri la mazao yake kwa kushirikiana na wadau wengine ambapo kwa upande mwingine ingepaswa kuishauri serikali kufufua viwanda vya nguo vilivyokufa ili kuweza kuongeza hitaji la pamba.
Tofauti na matarajio ya wakulima kutetewa na bodi, chombo kilichoundwa kwa ajili ya kumsaidia kimemtelekeza bila ya msaada wowote huku wakidai kwamba imegeuka kuwa mzigo kwa mkulima.
CCM ina kila sababu ya kufuatilia kilio hicho kwa kuangalia iwapo ni kweli bodi hiyo imesahau wajibu wake na badala yake imejikita katika masuala mengine, vinginevyo wakulima watashindwa kukielewa chama hicho iwapo kitakaa kimya bila ya kutoa tamko lolote.
Wakulima wamekuwa wakilalamikia kitendo cha kuporomoka kwa bei ya zao la pamba kila pale kinapofika kipindi cha mauzo ambapo wamekuwa wakihoji miezi michache kabla ya kuanza kwa msimu, bei ya pamba katika soko la dunia huwa ni ya juu lakini muda mfupi baada ya kufunguliwa kwa msimu bei hushuka ghafla.
Wanasema CCM inapaswa kuhakikisha mkulima anaondokana na kero hiyo ya kuporomoka kwa bei ya mazao yake kila mwaka na kwamba sasa inatakiwa kuvielekeza vyombo vyake vya utekelezaji (serikali) kutafuta mbinu mbadala itakayoweza kuinua bei ya mazao ya mkulima badala ya kutegemea kuuza mazao ghafi nje ya nchi.
Ndani ya ilani yake ya uchaguzi chama hicho kinaeleza wazi dhamira yake ya kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo ambayo ilinadiwa kwa wananchi katika mikutano mbalimbali ya kampeni mwaka 2010.
Ibara ya 225 inaeleza kwamba mara kwa mara CCM imekuwa inaelekeza vyema kazi ya Chama ya kuongoza na kusimamia kwa vitendo shughuli za chama na serikali. Pamoja na ukweli kwamba maelekezo yatolewayo ni mazuri, lakini utekelezaji wake umekuwa ukilalamikiwa.
Ibara hiyo inaeleza kwamba moja ya sababu ya mapungufu katika utekelezaji ni Chama kutotimiza jukumu lake la kuongoza kikamilifu kwa kuweka medhodolojia sahihi za kufuatilia, kudhibiti na kufanya tathmini.
Utekelezwaji kikamilifu wa ilani ya uchaguzi ndiyo njia pekee itakayoweza kukisaidia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuongoza dola bila tatizo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa vile itakuwa na cha kueleza kwa wapiga kura.
Hata hivyo iwapo CCM itashindwa kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa ilani yake ya uchaguzi kwa kuruhusu wananchi kuendelea kukabiliwa na kero mbalimbali kutokana na serikali yake kutozipatia ufumbuzi kero za wananchi ni wazi chama hicho kinaweza kujikuta kikiwa chama kikuu cha upinzani baada ya uchaguzi huo.
Zipo dalili ambazo si nzuri hivi sasa ambazo zimeanza kujionesha kwamba wananchi wengi wameanza kupoteza imani na chama chao walichokikabidhi dhamana ya kuongoza serikali ambapo kadri siku zinavyokwenda kumekuwepo na malalamiko mbalimbali ya wananchi ikiwemo wakulima kukosa masoko ya uhakika ya mazao yao.
Hata hivyo hatari kubwa inayokinyemelea chama hicho ni kitendo cha serikali yake hivi sasa kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wananchi katika halmashauri mbalimbali nchini baada ya kusitisha upelekaji wa fedha za ruzuku kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Halmashauri nyingi kuanzia kipindi cha mwaka 2010/2011 mpaka sasa zimeilalamikia serikali kuu kwa kitendo chake cha kushindwa kuzipelekea ruzuku ya fidia ya vyanzo vyake vya mapata vilivyofutwa hali ambayo imesababisha miradi mingi ya maendeleo iliyokuwa itekelezwe katika kipindi hicho kushindwa kukamilika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa nchini (LAAC) iliyotolewa hivi karibuni bungeni, kiasi cha shilingi 2,274,157,800,000 zilitengwa katika bajeti ya 2009/2010 kama ruzuku ya maendeleo na matumizi ya kawaida katika halmashauri 133 nchini, lakini hata hivyo hazikuweza kupelekwa kama ilivyopangwa.
Wakati serikali ikisitisha upelekaji wa fedha hizo za ruzuku katika halmashauri za wilaya hivi karibuni katika kile kilichoelezwa ni katika juhudi za kutaka kumsaidia mkulima wa zao la pamba kupata bei nzuri iliziagiza halmashauri zote ambazo hukusanya ushuru kutoka kwa wanunuzi wa zao pamba kushusha viwango vya ushuru wake.
Baada ya kutokea mvutano mkali kati ya wakulima wa zao la pamba, wanunuzi wa zao hilo na Bodi ya pamba kuhusiana na anguko la bei ya pamba, serikali iliagiza kupunguzwa kwa ushuru uliokuwa ukitozwa na halmashauri kwa wanunuzi wa zao hilo kutoka asilimia tano iliyokuwa ikitozwa kwa kila kilo moja ya pamba iliyonunuliwa hadi asilimia mbili.
Agizo hili limelalamikiwa na halmashauri zote ambazo hutegemea kwa kiasi kikubwa mapato yake ya ndani kutoka katika ushuru huo unaokusanywa kutoka kwa wanunuzi wa pamba katika maeneo yao ambapo wawakilishi wa wananchi (madiwani) wameelezea wazi kwamba miradi mingi ya maendeleo iliyokwisha andaliwa kwa mwaka huu itakwama.
Hata hivyo hivi karibuni kikao cha Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita (Bukombe) kiliamua kuunda timu ya watu saba ambao watakwenda kukutana na Waziri Mkuu ili kuishauri serikali ibadili uamuzi wake.
Mwenyekiti wa ALAT, Bw. Pius Machungwa anasema kitendo cha serikali kuzitaka halmashauri kupunguza kiwango cha ushuru kinachowatoza wanunuzi wa pamba katika halmashauri zao kitasababisha halmashauri hizo hivi sasa kupata hasara ya shilingi bilioni 6.1 na kuathiri kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Bw. Machungwa anasema mbali ya kushindwa kutekeleza mipango ya maendeleo, lakini pia halmashauri hizo zitashindwa kulipa mishahara ya watumishi wake wanaolipwa kwa kutumia mapato ya ndani, kuendesha vikao vya kikatiba, posho za madiwani za kila mwezi na huduma muhimu za uendeshaji ikiwemo ununuzi wa shajala za ofisi.
Anasema serikali katika kutoa agizo hilo haikufuata utaratibu kwa vile halmashauri husika hazikushirikishwa katika kufikia maamuzi hayo na pia haikueleza njia mbadala ambazo zitatumika kufidia pengo litakalojitokeza kwa vile halmashauri zote zilikuwa zimeishapitisha bajeti zake za mwaka 2012/2013.
“Lakini pia timu hii itakayokwenda kwa waziri mkuu itaelezea kwa kinagaubaga madhara ambayo halmashauri itakumbana nayo kutokana na agizo hilo la serikali kwa vile halmashauri zetu hutegemea zaidi mapato yanayotokana na ushuru unaokusanywa kutoka kwa wanunuzi wa pamba kwa zaidi ya asilimia 50,”
“Tutaiomba serikali itueleze baada ya kupunguzwa kwa viwango hivyo vya ushuru, wakati pia ikiwa imeshindwa kutopatia ruzuku ya fedha za maendeleo kwa vyanzo vya mapato vilivyofutwa na serikali yenyewe, hivyo itueleze miradi ya maendeleo tuliyoipitisha itatekelezwa kwa fedha kutoka wapi, maana wananchi hawatatuelewa wakiona miradi yao inadorora,” anaeleza Bw. Machungwa.
Ni wazi kwamba serikali ya CCM sasa inapaswa kukaa chini na kuangalia ni maeneo yapi ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ya haraka ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wake unatekelezwa kama ilivyokuwa imepangwa.
Namalizia makala hii kwa kurejea katika ilani ya uchaguzi ya CCM, sehemu ya ibara ya 227 ambayo inaeleza kwamba, “Kimsingi utekelezaji wa Ilani hii utafanikiwa kama Chama kitatekeleza jukumu lake la kusimamia kwa kuhakikisha kuwa program ya utekelezaji inaandaliwa na kusimamiwa ipasavyo,”
“Inawezekana kujenga Maisha Bora kwa kila Mtanzania na Tanzania yenye neema tele kama uongozi wa sasa wa Chama utabadilika kiutendaji, kimsimamo na kimtazamo.” Kwa hali hii uongozi wa CCM hivi sasa unatakiwa kuhakikisha unaisimamia kikamilifu serikali yake na kutowaonea aibu watendaji na hata viongozi ambao watabainika kwenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment