07 August 2012
CHANETA yapiga faini timu nne
Na Amina Athumani
CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kimezipiga faini ya sh. 100,000 timu nne kila moja kutokana na kushindwa kukamilisha taratibu za ushiriki wa mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza kwa wakati.
Timu zilizolimwa faini hiyo ni Magereza Morogoro, Polisi Mbeya, POlisi Dar es Salaam na Kambagwa Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji cha CHANETA, Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi alisema kikao hicho kilikuwa kikitoa maamuzi ya kuzifungia timu hizo au kuzipiga faini.
"Katika kikao cha leo (jana) tulikuwa tumeadhimia kuzifungia timu hizi lakini katika kujadili tukaona tusizinyime haki ya msingi ya kuzifungia bali zishiriki kwa kulipa faini ya sh. 100,000 kila moja,"alisema Mkisi.
Alisema pamoja na faini hiyo wamezitaka timu hizo ifikapo keshokutwa ziwe zimekamilisha taratibu zote za mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kukamilisha usajili wa wachezaji, kulipia vitambulisho na mambo mengine ya mashindano hayo.
Katibu huyo alisema pia kikao hicho kimepitia kwa umakini fomu za usajili zilizowasilishwa na timu 15 zilizothibitisha tangu awali kwa ajili ya kuzipitia ili ziweze kuendelea na utaratibu unaofuata.
Alisema kila timu imetakiwa kusajili wachezaji 21 katika kila msimu na kwamba wachezaji wanaotakiwa kuingia uwanjani ni 21 kwa mujibu wa kanuni na sheria za mashindano hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment