27 August 2012

Dkt. Slaa amtuhumu Kikwete




Na Goodluck Hongo, Morogoro

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kusaini posho, marupurupu ya wabunge na kushindwa kuongeza mishahara ya watumishi wa kada nyingine, kinaweza kuing'oa Serikali yake madarakani.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Willibrod Slaa, aliyasema hayo juzi katika mikutano ya hadhara aliyoifanya kkwenye vijiji vya Kata za Mvuha na Mtamba, Wilaya ya Morogoro, Kusini Mashariki.

Alisema kama Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), itaendelea kukandamiza makundi mbalimbali ya kijamii hasa wafanyakazi, wakulima, wafugaji na kukwepa kujadili vyanzo vya matatizo waliyonayo muda mrefu, wananchi wataiweka kitanzini.

“Rais Kikwete amekuwa akiidhinisha mishahara mikubwa na marupurupu mengi kwa wabunge hadi kufikia sh. milioni 11 kwa mwezi lakini anawaambia watumishi wa kada nyingine kuwa Serikali yake haina fedha za kuwalipa,” alisema Dkt. Slaa.

Aliwataka wafanyakazi wote nchini, kuendelea kuibana Serikali ili iweze kuwajibika kwa kutatua kero zao. “Juzi nimesoma kwenye mtandao na kuona walimu wakitumiana ujumbi.

“Kama ujumbe huu wataufanyia kazi, watoto wetu ambao wapo shuleni, hawataambulia kitu kwani ujumbe huo unawataka walimu wafundishe uongo mtupu wawapo darasani, hii ni ishara ambayo inaonesha wana kinyongo cha madai yao kupuuzwa na Serikali  hivyo Taifa linaweza kuangamia,” alisema.

Aliwaomba walimu katika mikoa yote nchini kupunguza hasira na kuwataka wasihamishe hasira zao kwa wanafunzi ambao hawana makosa ambapo kila mtu mwenye akili timamu, anafahamu kuwa madai yao ni ya msingi na adui yao mkubwa ni Serikali.

Dkt. Slaa alisema, yeye anatambua uhalali wa madai ya walimu lakini Rais Kikwete anawaambia wananchi kuwa Serikali haina fedha za kuwaongezea mishahara na kuwa lipa posho ambazo zinatokana na mazingira magumu ya kazi.

Wakati huo huo, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, kutengua ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga, mkoani humo, Dkt. Peter Kafumu (CCM), leo Dkt. Slaa atafanya mkutano wa hadhara jimboni humo.

Lengo la mkutano huo ni kuwashukuru wakazi wa jimbo hilo kwa kuonesha ushirikiano tangu mwanzo wa kesi ambayo iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wao, Bw. Joseph Kashindye.

Katika kesi hiyo, mgombea huyo alikuwa akiwakilishwa na wakili Profesa Abdallah Safari, ambaye aliwasilisha hoja 15 za kupinga ushindi wa Dkt. Kafumu.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho, ilidai Dkt. Slaa atafuatana na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Tabora, Kansa Mbaruku na baadhi ya maofisa ambao wanashiriki Operesheni Sangara (M4C) inayoendelea mkoani Morogoro.

Baada ya mkutano huo, timu hiyo itarejea mkoani Morogoro ili kuhitimisha opersheni waliyoianza kwa kufanya mkutano wa hadhara ambao utafanyika kesho kutwa.

No comments:

Post a Comment