23 August 2012
Kasoro hizi ziondolewe kufanikisha sera ya Kilimo Kwanza nchini
Na Faida Muyomba
HIVI karibuni Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Edward Lowassa, alinukuliwa na vyombo vya habari kuwa sera ya Kilimo Kwanza haitafanikiwa endapo wananchi hawatapatiwa elimu.
Bw. Lowassa, alitoa kauli hiyo mkoani Morogoro katika harambee ya kuchangia ujenzi katika shule ya msingi Ujirani iliyopo kata ya Mkundi katika Manispaa ya Morogoro.
"Tunapozungumzia Kilimo Kwanza, tuzungumzie suala la elimu kwanza,ukiwekeza kwenye elimu atatoka mkulima bora, hivyo serikali inatakiwa kuwapatia elimu wakulima ili waweze kutekeleza sera hii bila ubabaishaji,"anasema Bw. Lowassa.
Kauli hii imelenga kuwasaidia watanzania ambao wengi wao wanaishi vijijini wanaotegemea kipato chao kupitia kilimo ingawa hawana elimu ya juu ya nini wanatakiwa kukifanya ili kufanikisha sera hii.
Huu ni ukweli usiopingika na kila Mtanzania anatambua kuwa Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa letu japokuwa walio wengi hususani wasomi wanakibeza na kukiona kama kimebaki cha watu maskini wasio na elimu.
Watu wengi hawajui kuwa kilimo kikitiliwa mkazo kitachangia kuinua uchumi wa nchi licha ya kuwa kitapunguza tatizo la njaa kwa wananchi wake.
Kutokana na kutambua jambo hilo, serikali imeamua kuanzisha sera hiyo, lengo likiwa ni kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
Katika kudhihirisha azma hii ya serikali, Rais Jakaya Kikwete, wakati wa uzinduzi wa sera hiyo mwaka 2009, anasema imekusudia kuongeza kasi ya mapinduzi ya kilimo.
Anasema, Kilimo kwanza itakuwa mhimili muhimu katika kutekeleza dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya Rais ya uzinduzi sera ya Kilimo Kwanza, ni kwamba ilibuniwa chini ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambao ni mfumo wa mashauriano kati ya sekta ya umma na binafsi.
Takwimu zinaonesha kuwa, Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo, lakini ni asilimia 23 tu ndiyo inayotumika huku hekta milioni 29 kati ya hizo ndizo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Sera hii ilikuwa na nguzo kadhaa zikiwemo kukuza kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa wakulima wadogo hadi wakubwa pamoja na kuweka mkakati wa upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kilimo kwa masharti nafuu.
Nguzo nyingine ni kuboresha mipango ugawaji wa ardhi, kubuni sera za kuboresha mazingira ya uwekezaji, vivutio, utekelezaji mpango wa maendeleo ya viwanda, maendeleo ya rasilimali watu, matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuongeza matumizi ya pembejeo.
Matumizi ya mashine, miradi mikubwa ya kilimo cha umwagiliaji maji, barabara za vijijini na uhifadhi bora ili kupunguza hasara baada ya mavuno pamoja na kuimarisha masoko ya mazao ili mkulima apate soko la uhakika na bei zenye tija kulingana na jasho lake.
Kwa kuzingatia hayo, ndio maana tumeweza kuona sera hii ya Kilimo Kwanza ikitiliwa mkazo na serikali ambayo imeanza kwa kuzihimiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinafanikiwa kununua matrekta madogo maarufu kama 'Power Tillers'.
Matumizi ya matrekta yamelenga kuchukua nafasi ya jembe la mkono ambalo limekuwa kero kwa wakulima wengi nchini hivyo kukiona kilimo kama laana kwao.
Malengo ya serikali yalikuwa na manufaa, lakini kama anavyosema Waziri Mkuu Mstaafu Bw.Lowassa, bado elimu haijapatiwa kipaumbele kwa wakulima wetu.
Nasema hivo kutokana na ukweli kwamba, wakulima wengi hususani wale wa vijijini ambao ndio walengwa wakuu, hawajui lengo hasa la serikali kuamua matrekta yatumike katika kilimo.
Bila shaka sote tutakuwa mashahidi katika hili na hata wabunge wetu wamewahi kulizungumzia katika moja ya vikao vyao huko Bungeni mjini Dodoma hivi karibuni.
Kwa mfano, Mbunge wa jimbo la Geita,Bw. Donald Max, anasema kuwa matrekta hayo hayawasaidii wakulima.
Anasema kuwa, matrekta hayo madogo, yanafaa kulimia maeneo yenye udongo tifutifu kama vile Arusha, Morogoro na katika sehemu tambarare za Mkoa wa Shinyanga na kuwa hayafai kutumiwa maeneo yenye visiki na mawe kama huko Geita.
Anasema, kutokana na wakulima wengi kutokuwa na elimu juu ya matumizi ya matrekta hayo, wanayatumia kwa kusomba mawe na matofali hali inayochangia sera hiyo ya Kilimo Kwanza kuzidi kudorora na kutofikia malengo yake.
Pamoja na hayo bado asilimia 34 ya watanzania wengi wao wakiwa wale wanaotegemea zaidi kilimo, wanaishi katika hali ya umaskini.
Serikali kama ina nia ya dhati ya kutaka sekta ya kilimo kuwa mkombozi kwa watanzania na kuwa tegemeo kwa wananchi wake, inatakiwa kutoa elimu ya kutosha juu ya matumizi yake.
Mbali na wakulima kupewa elimu ya kutosha juu ya matumizi sahihi ya matrekta, pia serikali iandae mfumo madhubuti utakaosaidia wakulima hao kupata mikopo ya kununulia matrekta hayo madogo kwa gharama nafuu.
Nasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, wakulima wengi maisha yao yako duni mno hivyo kuwa vigumu kwao kununua matrekta hayo yanayouzwa kwa mamilioni ya fedha.
Bei kubwa kwa matrekta haya, kinaweza kuwa pia ni kikwazo cha kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa ya sera ya Kilimo Kwanza.
Nitoe mfano mmoja tu huko wilayani Geita, ambapo wadau wa kilimo wamesusia kuyanunua matrekta hayo kwa kile wanachodai ni masharti magumu ya ununuzi, ukopaji na namna wanavyotakiwa kumaliza deni.
Kutokana na hali hiyo, hadi sasa ukifika katika ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Geita, kuna idadi kubwa ya matrekta hayo zaidi ya 15 yakiwa yanaendelea kuozea pasipo kufanya kazi iliyokusudiwa na kubaki mapambo.
Halmashauri imefanya kazi ya kuyanunua na hatimaye kuyafikisha hapo tangu Mwezi Machi mwaka huu, lakini hakuna mkulima aliyekwisha jitokeza kununua japo kwa masharti yaliyowekwa na Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Said Magalula, anakiri kuwepo kwa hali hii wilayani humo, ambapo ameshauri Baraza la madiwani kufikiria upya mfumo wa uuzwaji ikiwa ni pamoja na kupunguza masharti yaliyowekwa.
"Nafikiri waheshimiwa madiwani chanzo cha wakulima kutojitokeza kuyanunua matrekta hayo kupitia mikopo kumechangiwa na masharti magumu yaliyowekwa, nashauri yalegezwe kama mnataka mpango huo utekelezeke ikiwamo namna ya umaliziaji deni na kiasi cha awali cha malipo," anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Mpangalutela Tatala, anasema kuwa trekta moja aina ya Farm track inayotengezwa na Suma JKT inauzwa kwa sh.milioni 31,000,500 ambapo mkulima anatakiwa kulipa kwanza sh.milioni 16 na kukamilisha kiasi kinachosalia katika muda wa miaka miwili.
Moja ya masharti kwa mkopaji ni kuwa na hati miliki ya nyumba, hali ambayo inakuwa ngumu kwa wakulima wanaoishi vijijini ambao nyumba zao hazina hati.
Hizi ni baadhi tu ya vikwazo vinavyoweza kuchangia kushindwa kwa sera hii ingawa yapo mambo mengi yanayotakiwa kushughulikiwa na serikali iwapo inataka ifanikiwe.
Mambo mengine mbali na hayo ni kuhakikisha inayafanyia kazi yale yote yaliyomo katika nguzo za Kilimo Kwanza, kama vile kuwe na barabara imara zinazoweza kupitika muda wote, wakulima waruhusiwe kutafuta masoko nje na ndani ya nchi.
Elimu ya matumizi ya mbolea mashambani iwe kama wimbo kwa wakulima wetu, itolewe ruzuku ya kununulia dawa za kuua wadudu na zaidi wale walioko karibu na ziwa wapewe elimu juu ya kilimo cha umwagiliaji.
Hivyo basi naishauri serikali endapo inataka kufanikiwa kubadilisha maisha ya watanzania kupitia sera hii, ni lazima izifanyie kwa vitendo nguzo kumi ilizojiwekea na si kubaki kama wimbo usiokuwa na waimbaji kwani itakuwa ni kazi bure.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment