23 August 2012

Uteuzi wa Bw. Utouh umoja wa Mataifa,uwe wa faraja kwa watanzania.



Na Michael Sarungi

HIVI karibuni Tanzania imeiingia katika historia ya Kimataifa kwa mara nyingine baada ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali(CAG) Bw.Ludovick Utouh, kuchaguliwa kuwa Mkaguzi wa Umoja wa Kimataifa.


Bw.Utouh, ambaye hivi karibuni amejizolea sifa kwa kuwa muwazi katika kazi zake, ameshika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Afrika Kusini, baada ya utumishi wake katika nafasi hiyo kufikia ukomo Juni 30 2012.

Kutokana na kuufahamu uwezo na uadilifu wake, wadau mbalimbali wameungana kuhakikisha kuwa mtaalamu huyo toka Tanzania anapata nafasi hiyo.

Hivyo mhusika anatakiwa aoneshe uwezo mkubwa na uwazi katika kazi yake ya ukaguzi.

Kwa kifupi nafasi hiyo inahitaji kuwa na taaluma zaidi ya uhasibu kama ilivyozoeleka kwa watu wengi na kuchaguliwa kwake ni sifa kwa nchi yetu na bara la Afrika kwa ujumla.

Hii ni inatokana na kazi kubwa na ushawishi uliofanywa na Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kushirikiana na Waziri wa Mambo ya nchi za nje Bw. Benard Membe.

 Bw. Utouh,aliteuliwa kuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia  umoja wa nchi za Afrika(AU),mwezi Mei mwaka jana.

Baada ya jina hilo kupitishwa na Umoja huo, kikwazo kikubwa kilikuwa ni katika  kamati ya tano ya Umoja wa Mataifa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Bw. Utouh alikivuka bila ya matatizo.

Baada ya hapo, Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilipokea mapendekezo ya kamati ya tano, ndipo kazi kubwa ikafanyika Chini ya Katibu Kiongozi Balozi Sefue Ombeni, kuhamasisha mataifa mengine kuiunga mkono Tanzania na Baraza likapitisha jina lake kwa azimio la Umoja wa mataifa New-York la mwezi Novemba,2011.

Bodi hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1946, inaundwa na wakaguzi wa hesabu za Serikali tatu kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kwa sasa wajumbe katika Bodi hiyo ni China, Uingereza na Tanzania na kabla ya hapo Afrika Kusini ilikuwa mjumbe hadi Julai Mosi mwaka huu.

Katika Bara la Afrika, nchi zilizowahi kupata nafasi hiyo, ni pamoja na Ghana iliyoshika kwa vipindi vya miaka 24, Afrika Kusini kwa miaka 12 na Tanzania itakayofanya kazi hiyo kwa miaka 6.

Mtaalamu huyu toka Tanzania, anachukua nafasi hii nyeti, wakati Umoja huo ukiwa unakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile utengenezaji wa mifumo bora ya kiutendaji wenye uwazi.

Changamoto nyingine ni uandaaji wa Bajeti zinazotegemea matokeo na vipaumbele, uboreshaji utendaji wa kazi pamoja na rasilimali watu.

Pia utekelezaji wa mifumo wa hesabu kwa utumiaji viwango vya hesabu vya umma (IPSAS) na uboreshaji wa ununuzi wa kidunia, ukosefu wa amani sehemu nyingi duniani, mahitaji kuwa mengi kuliko upatikanaji wa fedha.

 Rasilimali za uendeshaji na mabadiliko ya hali ya hewa duniani kote na hivyo kusababisha maeneo mengi hususani katika nchi nyingi za kiafrika kukabiliwa na njaa.

Kazi mpya ya Bw. Utouh, itafanywa na wakaguzi toka nchi tatu wanachama kwa kugawana maeneo ya kukagua na baada ya ukaguzi kukamilika kazi hiyo itaaputiwa na wakaguzi wakuu toka nchini China, Uingereza na Tanzania.

Kwa pamoja Wakaguzi wakuu watazipitia na kisha kuweka saini zao na kuziwasilisha katika kamati ya Umoja wa Mataifa.

Ili kufanya kwa umakini kazi hiyo, wajumbe hao wamegawana maeneo ya kusimamia ambapo Bw. Utouh atasimamia na kufanya ukaguzi katika taasisi za Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Misaada na Uokoji kwa Wapalestina (UNRWA), Shirika la kusimamia amani nchini Congo (MONUSCO).

Taasisi nyingine ni Shirika la kusimamia amani nchini Haiti (UNSTAMH),  Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu wa Kimataifa ya Yugoslavia (ICTY), Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Mauaji ya Rwanda (ICTR), Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UNW), Kundi la kulinda amani nchini Liberia (UNMIL) na kundi la amani nchini Somalia (AMILSON).

Ukaguzi huo unatarajiwa kuwa na watumishi 60 kati ya hao 24 ni wanawake na 36 ni wanaume ambao watahusika moja kwa moja katika kazi hiyo.

Kati ya watumishi hao, wawili wanatarajiwa kuhamia nchini Marekani  kumwakilisha Bw. Utouh,na wengine watakuwa wanafanya kazi kwa muda na kisha kurejea nyumbani.

Kwa upande wake, Bw. Utouh atakuwa akifika nchini humo, katika mikutano ya Bodi ya Ukaguzi ya Umoja Mataifa inayohusisha uwekaji wa saini na ripoti zitakazokuwa zikitolewa kila mara.

Hii ni tofauti na watu wengine wanaofikiria kuwa Mkaguzi huyo sasa anahamia nchini Marekani moja kwa moja.

Ili kuhakikisha kuwa wanafanya kazi hiyo mpya  kwa ufanisi, watumishi wote walioteuliwa kufanya kazi hiyo, walipewa mafunzo maalumu yaliyofanyika mwezi Machi mjini Arusha, na Dar es salaam mwezi Aprili na Mei mwaka huu.

Mafunzo haya yalienda sambamba na mafunzo ya vitendo kwa watumishi hao kushiriki katika ukaguzi uliokuwa ukiendelea wa Umoja wa Mataifa.

Julai 25 mwaka huu,Bw. Utouh akakabidhiwa uanachama wa ukaguzi wa Umoja Mataifa nchini Marekani.

Uteuzi huo ni kutambuliwa kwa utendaji wake ambao amekuwa akiuonesha katika nafasi aliyonayo  hapa nchini.

Hakika haya ni mafanikio  makubwa ambayo watanzania sibudi kujivunia, kwani haikuwa kazi rahisi kwake bila uzalendo na ushirikiano toka kwa watanzania wenzake.

Ni matumaini ya watanzania kuwa nafasi hiyo itamwezesha kuendeleza yale yote mazuri katika ukaguzi kwa maendeleo ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kuitangaza Tanzania ili iwe mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine duniani.




No comments:

Post a Comment