21 August 2012
Ilala yatenga mil. 474/- za kutoa elimu kwa jamii
Na Heri Shaaban
MANISPAA ya Ilala, Dar es Salaam, imetenga sh. milioni 474 ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu watoto wa mitaani na jinsi ya kuondokana na tatizo hilo.
Akizungumza na Majira juzi, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bw.Gabriel Fuime, alisema elimu hiyo itatolewa kupitia mradi wa Benki ya Dunia ambao unaitwa Dar es Salaam Metropilitan Development Project (DMDP).
“Manispaa hii inakusudia kutoa elimu juu ya tatizo la ongezeko la yatima linavyoendelea kukua, utafiti unaonesha kuwa asilimia 5.4 ya watoto wenye umri kati ya miaka 5-15 nchini wanaishi mitaani,” alisema Bw.Fuime.
Alisema mradi huo utasaidia kutoa elimu kwa jamii ili kukabiliana na ongezeko la watoto hao mitaani pamoja na kujenga ofisi za Serikali za Mitaa na kata ili zitumike kushughulikia tatizo hilo.
Bw.Fuime aliongeza kuwa, utawala bora ni nguzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi ili wananchi waweze kuibua, kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali katika maeneo yao.
“Viongozi ambao watasimamia mradi huu, watapewa mafunzo ya utawala bora ambapo kupitia Serikali za Mitaa, itatolewa elimu ya kupambana na rushwa kwa jamii,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment