21 August 2012

Kijiji hakina serikali miaka miwili


Na Yusuph Mussa, Kilindi

WAKAZI wa Kijiji cha Nkama, Kata ya Song, Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, wamesema kijiji hicho hakina Serikali kwa miaka miwili sasa baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wao, Bw.Shehe Gota, kufungwa jela kutokana na ubadhirifu wa fedha za wananchi.

Walisema Bw.Gota alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja ambapo aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bw.Khatib Lusewa, alihamishwa kituo cha kazi.

Wakazi hao waliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Suleiman Liwowa, ambaye alikwenda kijijini hapo kusikiliza mgogoro uliopo kati ya wakulima na wafugaji.

“Mkuu wa Wilaya, hapa kijijini hatuna Serikali ya kijiji zaidi ya miaka miwili sasa, Mwenyekiti wetu Bw. Gota alifungwa jela mwaka mmoja lakini aliyekuwa Ofisa Mtendaji, Bw.Lusewa alihamishwa kituo cha kazi.

“Tumebaini viongozi wa kata na halmashauri, wanawalinda wabadhirifu wa fedha za wananchi, tumeshangaa Mwenyekiti amefungwa haraka lakini Ofisa Mtendaji alihamishwa kituo, tunataka aturudishie mali zetu,” alisema Bw.Hassan Samaeli.

Diwani wa Kata ya Songe, Bw.Idrissa Mgaza, alisema uongozi wa kata haumtetei mtu ila taratibu na sheria ndiyo zinatumika ambapo suala la Mtendaji na wenzake lipo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), likifanyiwa kazi.

Kaimu Mkuu wa TAKUKURU, wilayani hapa, Bw.George Njogoro, alisema suala la kuwajua viongozi wa kijiji hicho kama wamefanya ubadhirifu wa fedha za wananchi linafanyiwa kazi ngazi za juu na kudai kuwa, kesi iliyomfunga Bw.Gota ni tofauti na hiyo wanayoshughulikia wao.

Akizungumza na wananchi hao, Bw.Liwowa amempa wiki moja Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi.Bibie Mnyamagola, awe ameweka Serikali ya muda katika kijiji hicho.

“Haiwezekani wananchi wakae bila Serikali kwa miaka miwili kwani jambo hilo litazorotesha maendeleo na usalama utakuwa mdogo, kama hakuna uongozi kijiji hiki kinaweza kuwa na matukio mengi ya uhalifu na hakiwezi kuwa na maendeleo,” alisema.

Bi.Mnyamagola alisema mchakato wa kufanya uchaguzi kamili wa kuwapata viongozi wapya wa kijiji utafanyika baada ya Sensa ya Watu na Makazi ambapo suala la kumuhamisha kituo cha kazi Bw.Lusewa linafanyiwa kazi na TAKUKURU.



No comments:

Post a Comment