28 August 2012

Halmashauri ziwe makini na fedha za miradi - RC



Na Agnes Mwaijega

HALMASHAURI zote jijini Dar es Salaam, zimetakiwa kuwa makini na usimamizi wa fedha na miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha zinafuata sheria ya manunuzi na malipo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Sadick Meck Sadik, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo.

Wajumbe hao walikuwa wakijadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Bw. Sadik alisema ripoti ya CAG imeonesha kuwa, yapo matumizi mabaya ya fedha za umma katika halmashauri hizo hali inayoashiria kuna utendaji mbovu.

Aliwataka Wakurugenzi wa halmashauri hizo kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria zilizopo na kufuata taratibu zinazotakiwa katika usimamizi vitengo vya manunuzi na malipo.

“Naomba utaratibu mbovu ukome kabisa kwa sababu unawatia mashaka wananchi na unazidi kudidimiza maendeleo ya miradi yetu,” alisema Bw. Sadik na kuwataka waache kutumia fedha ambazo si za kwao badala yake zipelekwe katika miradi husika.

Alisistiza kuwa, hatakuwa tayari kuwavumilia watendaji ambao hati zao zitaonekana kutokidhi viwango vya utendaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ilala, Bw. Mussa Zungu, alisema Wakurugenzi hao wanapaswa kupimwa upya kwa sababu baadhi yao uwezo wao kiutendaji ni mbovu.

“Tunataka kuwa na watendaji wenye uwezo wa kutunza na kutumia fedha za umma kwa kuzingatia sheria, upo umuhimu wa kila mtu aliyepewa jukumu la kusimamia miradi kuwajibika ipasavyo kwa umakini mkubwa,” alisema Bw. Zungu.


No comments:

Post a Comment