21 August 2012

EAC wajadili kupambana na uhalifu


Na James Gashumba, EANA

NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa Dkt. Julius Rotich, amesema upo umuhimu wa kuwepo juhudi za pamoja ili kuwadhibiti wahalifu wanaounda shirikisho lao kwa haraka kuliko nchi wanachama.

Alisema uhalifu wa kutumia mbinu za kisasa, unazidi kuongezeka kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira.

Dkt. Rotich aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akihutubia mkutano wa Wakurungenzi wa upelelezi, wasajili magari na wakuu wa vitengo vya kupambana na dawa ya kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu, Nairobi nchini Kenya.

“Umefika wakati wa wapepelezi kuibili changamoto hii ili kukabiliana na wahalifu pamoja na kuwatia hatiani,” alisema.

Aliongeza kuwa, mahitaji ya haki za binadamu na uwasilishaji  ushahidi ndani ya kanda hiyo, umeongeza shinikizo la kuwepo dhamira ya kuimarisha suala zima la upelelezi.

Alisema kutokana na umuhimu huo, Sekretarieti ya EAC imeweka kipaumbele cha kuanzisha Kituo cha Uchunguzi cha Kanda.

Bw. Rotich alidai kusikitishwa na taarifa za wataalamu kuwa wahusika wa biashara haramu ya dawa ya kulevya na usafirishaji  binadamu, wanatumia Kanda ya Afrika Mashariki kama njia kuu ya kufanya uhalifu huo.

Mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bw. Peter Kivuyo, amezitaka nchi wanachama kutoa adhabu kali kwa wahalifu wa dawa ya kulevya.

“Hivi sasa adhabu ambazo zinatolewa kwa wahalifu wa biashara ya dawa za kulevya au mawakala wao sio kali, haziwezi kuwaogopesha watu wengine kujiingiza katika biashara hii,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi nchini Rwanda, Bw. Christopher Bizimungu, alisema ushirikiano wa kubadilishana taaarifa za kiintelejensia katika EAC, umesaidia kuwatia mbaroni wahalifu wengi wa dawa ya kulevya.

“Ushirikiano huu umeleta mafanikio ya kudhibiti uhalifu wa biashara ya dawa ya kulevya katika kanda yetu,” alisema.


No comments:

Post a Comment