21 August 2012
Kanisa Katoliki lawataka waumini kushiriki sensa
Na Heckton Chuwa, Moshi
KANISA Katoliki Jimbo la Moshi, mkoani Kilimanjaro, limewataka waumini wake nchini kote kuona umuhimu wa kuhesabiwa na kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa ya Watu na Makazi.
Wito huo umetolewa jana na Padri Urbanus Ngowi wa Kanisa hilo katika Ibada ya Misa Takatifu, mjini hapa.
“Mkristo mzuri na mwaminifu ni yule anayezitii mamlaka zilizopo hivyo toeni ushirikiano katika mchakato huu ili kutimiza malengo ya Serikali yetu,” alisema Padri Ngowi.
Alisema matokeo ya sensa yana manufaa makubwa kwa Taifa kwani ndiop dira ya Serikali kupanga mipango ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wananchi wote.
“Tayari kuna taarifa kuwa, wapo baadhi ya watu wanaopotosha mpango huu wa Serikali, wito wangu kwetu watu wa aina hii wapuuzwe kwani dhamira yao si nzuri,” alisema.
Aliongeza kuwa, Serikali nia nzuri na wananchi wake hivyo Sensa ya Watu na Makazi ipewe kipambele kinachostahili na wote ambao watatoa visingizio ili kukwamisha mpango huo, watakuwa wamevunja sheria.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Sensa mkoani hapa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Leonidas Gama, Padri ambapo Padri Ngowi alitoa wito kwa waumini na wananchi wote kuliombea Taifa ili lizidi kuwa na amani.
“Hivi sasa mataifa mbalimbali yamekubwa na vurugu ambazo zimechangia wananchi wengi kupoteza maisha hivyo tufanye maombi ambayo yataepusha balaa hili,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment