21 August 2012

Dovutwa: Wabunge wala rushwa wafukuzwe


Na Grace Ndossa

MWENYEKITI wa Chama cha United People's Domocratic Party (UPDP), Bw.Fahmi Dovutwa, amesema vyama vyote vya siasa ambavyo wabunge wake wametuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa bungeni, vichukue hatua ya kuwawajibisha ili kujisafisha.

Bw.Dovutwa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema tuhuma za rushwa kwa wabunge ni aibu kwao binafsi na vyama wanavyotoka hivyo viongozi wa vyama husika, wanapaswa kuwawajibisha wabunge wao ili kulinda masilahi ya chama.

“Rushwa ni adui wa haki na inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya nchi na wananchi, kama vyama vyenye wabunge waliotuhumiwa kwa rushwa vitashindwa kuwawajibisha, wataadhibiwa na wananchi kwa kunyimwa ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.

“Kwa mfano, mke wa Kaisari alipotuhumiwa kuzini, aliundiwa tume ambayo ilimchunguza na kubaini kuwa hajazini lakini Kaisari bado alimuacha mke wake hivyo vyama hivi navyo vinapaswa kuwatosa wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa,” alisema.


Alisema kitendo cha wabunge kuomba rushwa ni kudhalilisha Bunge ambalo ndiyo chombo kinachotunga sheria.

Bw.Dovutwa alisema kauli ya Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda, aliyoitoa bungeni juu ya tuhuma za rushwa kwa wabunge, inashangaza kulingana na nafasi yake kwani alipaswa kuwasimamisha wabunge hao ili kupisha uchunguzi.

“Katika mihimili ya dola, hakuna chombo chochote ambacho ni kisafi iwe Serikali, Mahakama au Bunge,” alisema Bw.Dovutwa na kuunga mkono hoja ya wabunge wanaodai kuwa, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Bw. Edward Lowassa, hausiki na kashfa ya Richmond.

Alisema Waziri hana mamlaka ya kufanya jambo lolote bila ridhaa kutoka ngazi za juu kwani anapowajibika kufanya hivyo, anailinda Serikali iliyoko madarakani isianguke na uchaguzi kufanyika upya.

Aliongeza kuwa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alitoa ufafanuzi mzuri kuhusu suala zima la uwajibikaji lakini Watanzania wengi hawakumuelewa alipowarudisha kazini watumishi ambao walihusika na tuhuma mbalimbali.





No comments:

Post a Comment