21 August 2012

Hukumu Ubunge wa Kafumu leo *Mpinzani wake aliwasilisha hoja 13



Na Moses Mabula, Nzega

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora, leo inatarajia kutoa hukumu ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, yaliyompa ushindi mbunge wa sasa, Dkt.Peter Kafumu (CCM).

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw.Joseph Kashindye ambaye amepinga matokeo hayo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo, Bw.Protace Mgayane.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa Machi 26, mwaka huu na Jaji Mery Nsimbo Shangali.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Nzega, Bw.Silvester Kainda, alisema awali Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, ilipanga kutoa hukumu Agosti 20, mwaka huu, bahati mbaya ilikuwa sikukuu hivyo itasomwa leo.

Kwa upande wake, Wakili wa Mlalamikaji Profesa Abdallah Safari, alisema zaidi ya malalamiko 13 waliyawasilisha mahakamani hivyo wapo tayari kusikia uamuzi wowote ambao utatolewa.

Dkt.Kafumu anawakilishwa na mawakili wawili ambao ni Bw.Antony Kanyama na Bw. Kayaga Kamaliza ambapo miongoni mwa malalamiko yaliyowasilishwa na Bw.Kashindye ni pamoja na Bw.Kafumu kutoa vitisho, ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbuntu na kugawa mahindi.




No comments:

Post a Comment