21 August 2012
CHADEMA wavuna wanachama wapya 31,537 Morogoro
Na Goodluck Hongo, Morogoro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimevuna wanachama wapya zaidi ya 31,537 kutoka vijiji 271 vya majimbo saba yaliyopo mkoani Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Operesheni Sangara inayoendelea nchi nzima, Bw.Singo Kigaila, alisema jana chama hicho kimeendelea na ziara yake katika Jimbo la Kilombero, mkoani hapa.
Alisema hivi sasa wamebakiza majimbo matatu kumaliza operesheni yake mkoani hapa ambapo wananchi wameonesha kuikubali zaidi CHADEMA na kuichangia ili kuleta vuguvugu la maendeleo (M4C).
Aliongeza kuwa, tangu kuanza kwa operesheni hiyo mkoani humo Agosti 8 mwaka huu, chama hicho kimeweza kufungua matawi zaidi ya 100 ambapo hatua hiyo itawasaidia kuwa na takwimu sahihi za
wapiga kura wake.
Alisema katika operesheni hiyo, wamekabidhiwa kadi 7,605 za vyama vingine vya siasa nchini na kufanikiwa kuuza kadi zenye thamani ya sh.milioni 15.8 ambapo michango ya wanachama wanaokiunga mkono chama hicho ni sh.milioni 17.9.
“Baadhi ya wananchi wamekichangia chama chetu vipande 831 vya ndizi, magimbi 75, mchele kilo 148, mayai 17 na fenesi moja,” alisema Bw. Kigaila.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA upande wa Zanzibar, Bw.Said Issa Mohamed, aliwataka wakazi wa Morogoro kuona umuhimu wa kuhesabiwa ili Serikali iweze kujua idadi kamili ya wananchi wake na kupanga mikakati ya maendeleo.
“Sensa hii tunaiunga mkono kwani itakuwa msaada mkubwa kwa chama chetu pia, tunawaomba mtoe ushirikiano wa kuhesabiwa na kuondoa itikadi za kidini na vyama,” alisema.
Alisema Sensa ya Watu na Makazi ina maana kubwa kwani ndiyo msingi wa kupanga mikakati ya maendeleo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment