21 August 2012

Dkt.Slaa: Utatuzi migogoro ya ardhi Morogoro inahitaji busara ya serikali


Na Goodluck Hongo, Morogoro

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, ameiomba Serikali itumie busara kutatua migogoro ya ardhi hasa inayohusu mipaka katika Hifadhi za Taifa.


Alisema baadhi ya mipaka ya hifadhi hizo, ipo katika maeneo ya wananchi ambayo wameanza kuyamiliki muda mrefu hadi sasa.

Dkt.Slaa aliyasema hayo jana baada ya kufanya ziara katika majimbo sita ya uchaguzi mkoani Morogoro na kukuta kilio kikubwa cha wananchi ni migogoro ya ardhi.

Migogoro hiyo ni pamoja na ile inayohusu Hifadhi ya Mikumi na Udizungwa na kudai Serikali imekuwa ikitumia nguvu kubwa kuwaondoa wananchi katika maeneo waliyokaa muda mrefu.

Akizungumzia migogoro ya wakulima na wafugaji, Dkt.Slaa alisema viongozi wa Serikali ndiyo chanzo cha migogoro hiyo kwa kugeuza mtaji wao wa kujipatia fedha kutoka kwa wafugaji wanaoingiza ng'ombe kwenye mashamba ya wakulima.

“Katika migogoro hii, wakulima ndiyo waathirika wakubwa lakini Serikali inashindwa kutumia sheria iliyotungwa miaka minne ambayo imepita kuwatenganisha wakulima na wafugaji.

“Hadi sasa hakuna maeneo rasmi ya wafugaji na kama watashindwa kusimamia sheria husika, CHADEMA tutazunguka kuishtaki Serikali kwa Watanzania,” alisema Dkt.Slaa.

Aliongeza kuwa, viongozi wa Serikali za vijiji wameshindwa kuwasomea wananchi mapato na matumizi ya fedha za maendeleo na kuwafanya wananchi washindwe kujua Serikali Kuu imechangia kiasi gani ili kuboresha maisha yao.

Akizungumzia mbio za Mwenge wa Uhuru zinazofanyika kila mwaka, Dkt.Slaa alisema mbio hizo kwa sasa zimepoteza maana yake kama ilivyodhamiriwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere badala yake hivi sasa Mwenge unatumika kunufaisha baadhi ya watu pamoja na viongozi.

“Kipindi cha Mwalimu Nyerere Mwenge ulikimbizwa nchini ukiwa na maana ya kuwakumbusha Watanzania kuwa na upendo na kulinda amani iliyopo tofauti na ilivyo sasa.

“Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wamekuwa wakitozwa michango mingi ya kuendeshea shughuli za mwenge na wale
wanaoshindwa kuchanga wanatengwa,” alisema.

Alisema hakuna sheria inayolazimisha mtu kutoa mchango wa Mwenge hivyo Serikali iache mara moja kuwanyanyasa wananchi kwa kuwalazimisha watoe michango.

Dkt.Slaa alisema kama chama chake kitafanikiwa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu 2015, Mwenge ambao umekuwa na historia ndefu nchini, utapelekwa makumbusho ili watu waweze kufika na kupewa historia yake.



No comments:

Post a Comment