27 August 2012
CUF: Siasa chafu Arusha hatuzitaki
Na Said Njuki Arusha
CHAMA Cha Wananchi (CUF) mjini Arusha, kimewataka wakazi wa jiji hilo kuwa makini na siasa za kupakana matope ambazo haziwezi kuleta tija katika maisha yao.
Mwenyekiti wa Vijana wa CUF Taifa, Bw. Anthony Kanali, aliyasema hayo juzi wakati akihutubia wakazi wa mji huo katika kata ya Daraja Mbili na kuwataka waachane na propoganda za kisiasa kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
Alisema propoganda katika siasa hazina maana kwani mara nyingi hutumika kuwadanganya wananchi ambao hivi sasa, wamechoshwa na vitendo hivyo na kuamua kuiunga mkono CUF.
“Wapo wanasiasa wanaodiriki kutoa matusi kwa vyama vingine, nawahakikishia CUF ndio chama makini kilichobaki nchini, sisi hatuna siasa za kejeli kwa vyama vingine.
“Tupo imara kuendeleza siasa za kistaarabu ili kuwakomboa wananchi na kujiletea maendeleo, kwa muda mrefu jiji hili limekumbwa na misukosuko ya kisiasa.
“Vurugu hizo zimechangia kuvuruga mipango mingi ya kiuchumi na kutishia mustakabali wa maisha ya wananchi, ipo siku mtakuja kujuta kwa kushabikia siasa za aina hii,” alisema Bw. Kanali.
Aliongeza kuwa, propoganda za kisiasa ni hatari kwa uchumi wa mtu binafsi na Taifa lolote duniani kwani tangu zilipopenyezwa kwa waakazi wa jiji hilo, hali ya kiuchumi imezidi kuwa mbaya.
“Arusha ndiyo kitovu cha utalii nchini, ndipo kwenye soko kuu la madini ya vito, mazao ya kilimo, Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mahakama ya Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR), lakini umaskini bado unazidi kutikisa watu wake kutokana na siasa chafu,” alisema.
Awali Kaimu Katibu wa CUF Wilaya ya Arusha, Bw. Hassan Zani, alisema chama hicho kimevuna zaidi ya wanachama 3,000, katika kipindi kisichozidi miezi mitatu mjini hapa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment