21 August 2012
DC awataka wananchi kushiriki vikao
Na Mashaka Mhando, Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw.Mrisho Gambo, amewataka wananchi wilayani humo kuhudhuria vikao ambavyo vinaitishwa na viongozi wao wa vijiji.
Alisema kama watasusia vikao hivyo, watatoa mwanya kwa viongozi wao kutumia vibaya fedha wanazochanga na zile zinazoletwa na Serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali.
Bw.Gambo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kwagunda, akiwa ameongozana na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw.Stephen Ngonyani.
Aliongeza kuwa, lazima wananchi washiriki mikutano hiyo ili waweze kusomewa taarifa za mapato na matumizi ya fedha wanazochanga kutoka kwa viongozi wao.
Alisema ni haki kwa viongozi kuitisha mikutano mikuu ya vijiji kila baada ya muda unaotakiwa na kijiji husika ili kujadili mambo mbalimbali yakiwemo ya maendeleo.
Aliongeza kuwa, wananchi wanapohudhuria mikutano husika watasomewa taarifa za mapato na matumizi ili kuondoa malalamiko yanayotokea mara kwa mara juu ya matumizi mabaya ya fedha.
Bw.Gambo alilazimika kuyasema hayo baada ya viongozi wa kitongoji hicho kudai kuwa, changamoto kubwa waliyonayo ni pamoja na wananchi kutohudhuria vikao mbalimbali ambavyo wamekuwa wakiviitisha ukiwemo Mkutano Mkuu wa Kijiji wenye ajenda nyingi za maendeleo.
Alisema wananchi wanaoshindwa kuhudhuria vikao hivyo wanapata hasara kubwa kwani hawawezi kujua fedha zao zinatumika vipi hivyo kusababisha viongozi kutumia vibaya fedha za wananchi.
“Chonde chonde jamani nendeni kwenye vikao vya hawa viongozi, msisuse kwani mkisusa mnaopata hasara ni nyinyi kwa sababu hamtajua fedha zenu zinatumikaje.
“Msiporidhika na taarifa zinazosomwa, njooni mnieleze haraka hawa viongozi ni saizi yangu najua nitawashughulikia vipi,” alisema Bw.Gambo.
Kwa upande wake, Bw.Ngonyani alitoa fedha kwa taasisi za dini sh. milioni 1.2 ili ziweze kuimarisha makanisa na misikiti kijijini hapo.
Kati ya fedha hizo, sh. 500,000 zilitolewa kwa Kanisa la Kipentekoste ili kununulia vyombo vya muziki, Kanisa la Anglikana sh. 100,000, Kanisa Katoliki sh. 100,000 na msikiti uliopo katika kijiji hicho sh. 100,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment