27 August 2012

DAAA yatamba kung'ara mashindano ya Taifa



Na Amina Athumani

CHAMA cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAAA), kimetamba kufuta uteja katika mashindano ya Taifa ya mchezo huo na kwamba watahakikisha wanavunja rekodi kwa mkoa huo.

Michuano hiyo imepangwa kufanyika Septemba 7 na 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salam na kushirikisha wanariadha kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza wakati wa mchujo wa kwanza uliofanyika juzi katika viwanja vya Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Katibu Mkuu wa DAAA, Lucas Mkungu alisema mara nyingi ubingwa wa Taifa huchukuliwa na mikoa mingine kama Singida, Arusha na wanariadha wa Zanzibar huku mkoa wa Dar es Salaam ukishindwa kufanya vema.

Alisema kutokana na hali hiyo kwa mwaka huu wamejipanga kuhakikisha uteja huo wanafuta huku wao kama wenyeji wakihakikisha wanautumia vema uwanja wa nyumbani kubakiza ubingwa huo.

Alisema ili kufanikisha hilo wameanza maandalizi mapema na wamekuwa wakifanya mazoezi kila Jumamosi kwa kuwakutanisha vijana mbalimbali wa klabu za Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na wachezaji walioshiriki mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA.

Alisema wanatarajia kufanya mchujo wa mwisho Septemba Mosi, mwaka huu ili kupata kikosi kamili kitakaouwakilisha Mkoa wa Dar es Salaam katika mashindano hayo.

Alisema katika mchujo wa kwanza uliofanyika juzi ulishirikisha jumla ya vijana 30 ambao wote ni chipukizi na kwamba lengo ni kuhakikisha wanaziamsha damu changa zitakazokuwa zinaleta upinzani mkubwa katika michezo ya ndani na nje ya nchi kwa kuwa wanariadha wengi kwa sasa wameanza kupoteza uwezo wao.

No comments:

Post a Comment