31 August 2012

Bashe, Kigwangala watoleana bastola *Walikuwa wakirudisha fomu za NEC *Katibu CCM Nzega aamulia ugomvi



Na Allan Ntana, Nzega

KATIKA hali isiyo ya kawaida, wagombea wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, wanaowania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), wilayani hapa, wanadaiwa kutishiana bastola.

Wagombea hao ni Bw. Hussein Bashe na mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Hamis Kigwangala, ambapo tukio hilo limetokea juzi, katika ofisi za CCM, wilayani hapa.

Wakiwa katika ofisi hizo, Dkt. Kigwangala, anadaiwa kumwambia Katibu wa CCM wilayani hapa, Bw. Kajoro Nyohoroka, kuwa asipokee fomu iliyorejeshwa na Bw. Bashe kwani amechelewa kujaza na muda wa kuirejesha umekwisha.

Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mwanachama wa chama hicho (jina linahifadhiwa), ameliambia gazeti hili kuwa baada ya Dkt. Kigwangala kutoa agizo hilo, Bw. Bashe, alidaiwa kutoa matusi.

Kutokana na hali hiyo, Dkt. Kigwangala, alinyanyuka ghafla na kutaka kumpiga Bw. Bashe, huku akimtishia kumpiga risasi kwa bastola na mwenzake kutoa yakwake lakini ugomvi huo uliamuliwa.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wilayani hapa, Bw. Nyohoroka alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ofisini kwake.

Alisema awali Dkt. Kigwangala alikuwa ofisini kwake akijaza fomu ambapo Bw. Bashe naye alikuwa katika Ofisi ya Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Bw. Francis Shija.

Aliongeza kuwa, Bw. Bashe alirejesha fomu hizo saa 9:50 jioni ambapo Dkt. Kigwangala, alirejesha saa 9:48 na kulalamika mwenzake amechelewa kuiwasilisha hivyo isipokelewe.

“Baada ya hapo, yaliibuka maneno makali kwa wagombea wote, kutoleana vitisho na bastola,” alisema.

Akizungumza na Majira, Bw. Bashe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai Dkt. Kigwangala, alimtishia bastola akidai fomu yake isipokelewe kwani muda wa kuirejesha umekwisha.

“Muda ulikuwa haujaisha, huyu ndugu yangu ana visa na chuki dhidi yangu, ni kweli nilichomoa bastola lakini wanachama walituamua,” alisema Bw. Bashe.

Naye Dkt. Kigwangala aliliambia gazeti hili kuwa, hakuna kitu cha namna hiyo bali Bw. Bashe ni mzushi anayetaka kukuza mambo.

“Siyo kweli, hamna kitu cha namna hiyo...Bw. Bashe anataka kuyakuza tu ila ukweli ni kwamba, katibu amembeba, muda wa kurejesha fomu ulikuwa umeisha...nitakupigia baadaye,” alisema.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Antony Rutta, alithibitisha kuwa na taarifa za tukio hilo ila aliahidi kulifuatilia ili kujua chanzo.

“Kweli nimepata taarifa za tukio hili, hivi sasa nakwenda Kata ya Loya, wilayani Uyui, kufuatilia masuala ya sensa jinsi yanavyokwenda, nitalifuatilia,” alisema.




2 comments:

  1. yaaani siasa za ccm ni vurugu tupu huku wakikilaani chadema kwamba ni chama cha fujo. ni kiongozi gani wa chadema anatembea na silaha kiunoni? kama kweli serikali wanayoisimamia ni ya amani na jeshi la polisi linasimamia amani kikamilifu, kuna haja gani ya kila kiongozi kubeba silaha? utayakumbua ya Rage na pistol kiunoni kule Igunga. Utaiyakumbuka ya Malima na arsenal ya kivita kule Morogoro. Sasa haya. CCM ni aibu tupu!

    ReplyDelete
  2. Matokeo yake: Bashe atapigwa tena marufuku kwa utovu wa nidhamu na Dr. Khamis(kama kweli jina lake, maana tunaambiwa ni kihiyo kwani the really Khamis ni holder wa cheti halisi) atasubiri grace ya viongozi wa juu waliombeba 2010! Sooo funny! CCM kama haimtaki mtu bwana, itafanya kila mbinu!

    ReplyDelete