24 August 2012
AY, Papa Wemba, 2face jukwaa moja
Na Mwandishi Wetu
WANAMUZIKI nguli Afrika, wataungana na msanii mahiri wa kizazi kipya nchini Ambwene Yessaya, kutumbuiza wakati wa mechi ya fainali ya michuano ya Airtel Rising Stars, itakayopigwa kesho Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.
Nyota watakaotumbuiza katika fainali hiyo ni Papa Wemba wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), 2 Face Idibia wa Nigeria, Ambwene Yessaya na Daddy Owen wa Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na waandaaji wa michuano hiyo, wanamuziki hao wataanza kutoa burudani kuanzia mchana ambapo kila mmoja atatumbuiza nyimbo zilizompatia umaarufu ndani na nje ya nchi yake.
Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘African Queen’ na ‘If love is a crime’ za 2 Face Idibia, ‘Show me the way’ ya Papa Wemba na ‘Bed n Breakfast‘, ‘Goodlook’ na ‘Freeze’ za Ay.
Michuano hiyo iliyofunguliwa Jumatatu iliyopita na Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga imeshirikisha timu 15 za Afrika ambapo mechi yake ya fainali itaoneshwa moja kwa moja na Super Sports.
Nchi zilizoshiriki ni wenyeji Kenya, Tanzania, Madagascar, Malawi, Ghana, Zambia, Gabon, DRC, Burkina Fasso, Chad, Congo Brazaville, Uganda, Niger, Nigeria na Sierra Leone.
Katika hatua nyingine, habari kutoka Nairobi timu ya Tanzania ilikuwa nyuma kwa magoli 2-1 dhidi ya Zambia katika mchezo wa mwisho uliokuwa ukichezwa Uwanja Nyayo.
Kama matakeo yatabaki hivyo, vijana hao wa Tanzania watakuwa wameaga mashindano hayo, kwani mechi ya kwanza walichapwa bao 1-0 na Gabon kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Burkina Fasso.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment