16 July 2012

Yanga yaanza vibaya Kagame *Simba, Azam, Mafunzo zamu yao leo *APR yaichanachana El Salam Wau



Na Speciroza Joseph

MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga jana imeyaanza mashindano hayo vibaya baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi ya michuano hiyo iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mpira ulianza kwa kasi  kwa timu zote kupiga pasi za uhakika lakini kama mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza angekuwa makini angeweza kuifungia timu yake bao kwa kichwa lakini mpira ukatoka nje.

Dakika ya tisa na 13 Yanga ilihamia tena langoni mwa Atletico lakini wachezaji Jerry Tegete na Athuman Idd 'Chuji' mashuti yao yalipanguliwa na kipa Said Ndikumana aliyekuwa kikwazo kikubwa.

Baada ya mashambulizi hayo Atletico iliamka usingizi ambapo mshabuliaji wake Hassan Habizimana, aliyeogangana na beki mmoja wa Yanga aliachia shuti la mbali lililokuwa likielekea langoni lakini kipa Yaw Berko aliokoa kwa ustadi.

Dakika ya 35 Yanga ilipata kona tatu mfululizo ambapo kulitokea tafrani kubwa langoni mwa Atletico, baada ya wachezaji wa pande zote kusukumana kuwania mpira wa kona.

Kipindi cha pili Atletico iliingia na nguvu mpya ambapo iliweza kuikamata Yanga hasa sehemu ya kiungo na kuwafanya wachezaji wa Yanga kuwa katika wakati mgumu.

Katika kipindi hicho Yanga, ilimtoa Juma Abdula ambaye aliumia mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Ladislaus Mbogo na pia walitoka Tegete Rashid Gumbo na kuingia Nizar Khalfan na Said Bahanuzi.

Atletico nayo ilimtoa Claude Nahimana na akaingia Christian Mbilizi.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Atletico ambayo ilikuwa ikicheza soka safi kwa pasi fupifupi ambapo dakika ya 80 ilipata bao la kwanza kupitia kwa Didie Kavumbagu ambaye aliunasa mpira wa krosi iliyochongwa na Christopher Ndayishimiye.

Kabla ya Ndayishimiye kuachia krosi alifanya kazi nzuri kwa kuwatoka mabeki wa Yanga na kupiga mpira uliozaa bao hilo.

Hata hivyo kocha wa Atletico alimtoa nje mchezaji huyo na nafasi yake kuchukuliwa na Ciza Hussein na pia alitoka Mbazumatina na kuingia Olivia Nduwimana.

Atletico iliongeza bao la pili dakika ya 90 kupitia kwa Didie baada ya kuwatoka na mabeki wa Nadir Haroub 'Canavaro' na Mbogo na kuuwahi mpira ambapo aliupiga huku akimruka kipa wa Yanga, Berko na kuifanya timu yake kuibuka kidedea.

Katika mechi nyingine ya ufunguzi iliyopigwa saa 8 mchana katika uwanja huo, timu ya APR iliiadhibu El Salam Wau ya Sudan Kusini mabao 7-0.

Leo katika uwanja huo mabingwa wa Tanzania Bara Simba watajitupa uwanjani saa 10 jioni kumenyana na URA ya Uganda wakati mechi ya saa 8 mchana itakuwa kati ya Vita dhidi ya Ports.

Wawakalishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo Azam FC, itajitupa katika Uwanja wa Chamazi dhidi ya Mafunzo saa 10 jioni.

No comments:

Post a Comment