16 July 2012
Simba, Yanga, Azam, Mafunzo tupeni raha Kagame
MICHUANO ya Kombe la Kagame inaanza rasmi leo, huku tukiwashuhudia mabingwa wa tetezi wa kombe hilo wakicheza na Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
Yanga ni timu pekee ya Tanzania ambayo leo itakuwa uwanjani hivyo ni wakati mzuri kwao kuonesha uwezo wao katika harakati za kulibakisha kombe hilo nyumbani na si kuwaachia wageni.
Mwaka jana tulishuhudia Tanzania ikiiwakilisha vyema katika michuano hiyo, baada ya timu zote Simba na Yanga kuingia fainali, hivyo basi na mwaka huu tunataka kuona timu za Tanzania zikilibakisha tena kombe hili.
Wakati Yanga watashuka uwanjani leo wawakilishi wengine wa Tanzania Simba nao watakuwa na kibarua kesho, watakapocheza na URA ya Uganda, huku Azam FC wakimenyana na ndugu zao Mafunzo ya Zanzibar.
Mwaka huu tumepata bahati kubwa sana kwa Tanzania kuwakilishwa na timu nne, tatu za Bara na moja ya visiwani, hivyo tuitumie vizuri nafasi hiyo ili tuweze kulibakisha kombe nyumbani.
Pia ni nafasi nzuri kwa timu zetu kuonesha mashabiki wao vifaa vipya ambavyo vimesajiliwa msimu huu, kwani pia makocha watapata nafasi nzuri ya kutengeneza vikosi vyao, kabla ya kuanza mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Michuano hii inashirikisha mabingwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo kila timu ambayo imekuja inauwezo na si kuanza kuzibeza, kwani mpira unabadilika kiwango kilichooneshwa mwaka jana si cha leo tena.
Majira tunaamini kabisa hakuna vibonde katika michuano hiyo na timu zetu zikiweka imani hiyo zinaweza kujikuta zikipoteza nafasi kwa kudharau uwezo wa timu fulani na hivyo kujikuta wakiambulia vichapo.
Tunachukua nafasi hii kuzitakia kila la kheri timu zetu za Tanzania, na zaidi ya yote libakizeni kombe nyumbani, uwezo na nia mnayo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu zibariki timu zetu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment