17 July 2012

Yanga kutupa karata nyingine leo



Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga leo inashuka uwanjani kutupa karata yake nyingine dhidi ya Wau Salaam ya Sudan Kusini katika mfululizo wa mechi za michuano Kombe la Kagame, inayoendelea jijini Dar es Salaam.


Kabla ya timu hizo kutifuatana, utatangulia mchezo wa kukata na shoka kati ya wababe wa Yanga, Atletico ya Burundi itakayoumana na APR ya Rwanda katika mechi itakayoanza saa nane mchana.

Yanga ambao ndiyo mabingwa watetezi, watashuka uwanjani kutaka kufufua matumaini kwa wanachama na mashabiki wake, baada ya mechi ya kwanza kuchapwa mabao 2-0 na Atletico, hivyo itahitaji kushinda ili kujiweka pazuri.

Katika mechi hiyo, Yanga itahitaji ushindi ili kupata pointi tatu huku ikiziombea timu hizo zitoke sare kwani zitakuwa na pointi nne huku yenyewe ikiichapa, Wau itakuwa na pointi tatu.

Kama matokeo yakiwa hivyo, mechi za mwisho ambapo Yanga itacheza na APR na Atletico itaumana na Wau, zitakuwa na ushindani wa aina yake kwani hakuna timu ambayo ina nafasi ya moja kwa moja ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Akizungumzia michuano hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfeit alisema katika mchezo wa leo atajitahidi wachezaji wake wafanye vitu kama anavyovitaka tofauti na mchezo waliopoteza.

"Tulifungwa katika mechi ya awali kutokana na wachezaji wangu kutofuata kile nilichotaka wafanye, lakini ni makosa ambayo nitayafanyia kazi ili tufanye vizuri katika mechi zilizobaki," alisema Saintfeit.

Kwa upande wa mechi kati ya Atletico na APR, itakuwa na ushindani kwa kuwa kila moja itataka kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ili ipate tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo.

Atletico katika mechi ya kwanza iliichapa Yanga mabao 2-0 na APR ikaishushia mvua ya mabao 7-0 Wau Salaam.

Lakini kundi hilo kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, litatoa 'best looser', hivyo kati ya timu hizo zinaweza kuingia kwa kutumia nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment