02 July 2012
Yanga kucheza mechi mbili za kirafiki
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, Fredy Felix 'Minziro', amesema angependa kucheza mechi mbili zingine za kirafiki kabla ya kutetea ubingwa wao wa Kombe la Kagame ili kutoa nafasi ya kuwajua zaidi wachezaji wapya.
Alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya kumaliza kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya The Express ya uganda, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Minziro alisema timu yake imecheza vizuri na ndio maana imeibuka na ushindi lakini bado anahitaji mechi mbili zaidi ili kukiweka sawa kikosi chake kwa ajili ya Kombe la Kagame ambapo ana imani uongozi utalishughulikia suala hilo.
"Timu imecheza vizuri kwani kila mchezaji amejituma kadri awezavyo na hii inatokana na kila mmoja kuhitaji kupata namba katika kikosi cha kwanza," alisema Minziro na kuongeza;
"Wachezaji wapya wameonesha kiwango kizuri na ndio maana hata mashabiki waliokuwepo uwanjani walikuwa wakiwashangilia muda wote hususani Said Banahuzi amecheza vizuri sana."
Akizungumzia mchezaji huyo zaidi, alisema ni mchezaji mzuri ambaye ana uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mwisho na ndio maana katika mechi hiyo licha ya kutofunga lakini mabao yote ameyatengeneza yeye.
Yanga imepangwa Kundi C pamoja na APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kusini pamoja na Atletico ya Burundi ambapo watafungua michuano hiyo kwa kucheza na Atletico.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment