02 July 2012

Sumaye asikitishwa nchi kuporomoka kisoka *Azitolea uvivu Simba, Yanga



Na Zahoro Mlanzi

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesikitishwa na kupoteza umaarufu kwa soka la Tanzania ukilinganisha na miaka ya 1970.

Sumaye alisema hayo Dar es Salaam juzi katika hafla ya kuwatunuku washindi mbalimbali waliofanya vyema kwenye Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012.

Alisema hali hiyo inatokana na klabu nguli za Simba na Yanga, kubweteka kwa moja kuifunga mwenzake na kujiona zimefika peponi kitu ambacho si dalili nzuri katika maendeleo ya soka.

“Simba kuifunga Yanga au Yanga kuifunga Simba si kigezo kizuri cha kujiona ni timu nzuri, timu inatakiwa iangalie ushindani wa kimataifa …ndiyo maana hata wakipangiwa timu kutoka Misri, Ivory Coast zinaingiwa na hofu kubwa,”alisema na kuongeza.

“zamani klabu za nje zilikuwa zikipangwa na timu za Tanzania zinatetemeka lakini sisi sasa kama tunataka kurudi katika heshima yetu ya zamani tujipange kimataifa".

Pia Sumaye alisikitishwa na migogoro katika klabu na kusema inachangia pia kudidimiza soka, hivyo amewataka viongozi kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano sambamba na kuzihudumia ipasavyo klabu zao.

Sumaye ambaye ni mpenzi mkubwa wa mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba, alitumia fursa hiyo kuwaasa mashabiki na wanachama wa timu za Simba na Yanga kuzomeana uwanja pindi moja ya timu inapokuwa uwanjani.

“Muwe wapinzani katika michezo lakini si uhasama, lazima tuwe na urafiki baina yetu na kuonyesha uzalendo zaidi kwa Simba kuishangilia Yanga ikicheza na timu ya nje au Yanga kuishangili Simba ikicheza na timu ya nje,”alisema.

Sumaye pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza washindi wote na kuwataka kutovimbishwa vichwa na zawadi hizo badala yake wazitumie kama kichocheo cha kujibiidiisha zaidi.

Awali Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom, Kelvin Twisa alisema kampuni yake imetoa zaidi ya shilingi milioni 113 kama zawadi za washindi hao na hivyo kufanya mwaka huu zawadi kuongezeka tofauti na mwaka jana zilikuwa shilingi milioni 90.8.

“Tunajivunia kuwa wadhamini wa ligi kuu bara ambapo vipaji vingi vimeonekana na viwango vya kuvutia pia katika mechi zote na ndio maana hii leo tupo katika kutoa zawadi kwa washindi,”alisema.

Katika halfa hiyo, ilitambulishwa tuzo mpya inayohusisha wachezaji vijana waliofanya vyema kwenye timu hizo ambapo waliotwaa ni pamoja na Rashid Mandawa (Coastal Union), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting) na Frank Damayo aliyekuwa anaichezea JKT Ruvu na sasa amesajiliwa Yanga ambapo kila mmoja alizawadiwa shilingi milioni moja.

Azam Fc ilifanikiwa kuongoza kwa kutwaa tuzo tano ikiwemo ile ya nafasi ya pili iliyowapatia sh.mil.22, timu yenye nidhamu (mil.7.8), kocha bora-Stewart Hall (mil.3.8), mfungaji bora- John Bocco (mil.3.9) na mchezaji bora- Aggrey Morris (mil.3.3).

Aidha mabingwa Simba walitwaa mil.50, huku kipa wake Juma Kaseja alitwaa tuzo ya kipa bora na kuzawadiwa sh. mil 3.3, wakati Yanga ilizawadiwa mil.15 kwa kushika nafasi ya tatu na Martin Sanya alitwaa tuzo ya mwamuzi bora na kuzawadiwa mil.3.8.

No comments:

Post a Comment