02 July 2012

Serikali yahusishwa kumteka Ulimboka *CHADEMA yasema serikali haiwezi kujichunguza *Polisi yawaonya wadaktari waliogoma, watoa agizo



Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu (CHADEMA), amesema Serikali inahusika na tukio la kutekwa nyara Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka na kutaka wahusika wa tukio hilo wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Bw. Lissu alisema Serikali haiwezi kujitoa na tukio hilo ambapo tume iliyoundwa kuchunguza unyama huo, hawana imani nayo akidai Serikali haiwezi kujichunguza yenyewe

Bw. Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, alisema Serikali inapaswa kuunda tume huru ambayo itaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu na wajumbe wake watoke katika vyombo huru kikiwemo Chama cha Wanasheria na Taasisi nyingine za kitaaluma.

Alisema pamoja na Serikali kuchukua uamuzi wa kuwasimamisha kazi madaktari waliokuwa kwenye mgomo, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, amepotosha umma bungeni kutokana na maelezo yake kuwa Serikali haiwezi kutoa taarifa za mgogoro huo bungeni.

“Serikali imeamua kuwafukuza na kuwasimamisha kazi madaktari wa Hospitali za Bugando, Dodoma na Mbeya, Bw. Pinda alidai bungeni kuwa, Serikali haiwezi kujadili suala la mgomo wa madaktari kwa kisingizio suala hili liko Mahakamani,” alisema.

Aliongeza kuwa, kitendo cha Dkt. Ulimboka kumtambua Ofisa wa Polisi kwa alihusika na tukio la kutekwa kwake na kupigwa, Serikali inapaswa kumkamata ofisa huyo na kumfungulia mashtaka ya kumteka na jaribio la kutaka kumuua.

“Watu waliomteka ni polisi, sio majambazi kama inavyodaiwa ni watumishi wa vyombo vya dola...sisi hatuna imani na uchunguzi wowote wa Jeshi la Polisi, tunataka iundwe tume huru ambayo itaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Chama cha Wanasheria pamoja na wanataaluma,” alisema Bw. Lissu.

Alisema kauli ya Bw. Pinda kuwa suala hilo liko mahakamani, imelenga kuizuia Serikali isijieleze mbele ya Bunge kuhusu hatma ya mgomo wa madaktari nchini.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo Bw. John Myika (CHADEMA), alisema Katiba inatamka wazi kuwa bunge ndio chombo kikuu cha wananchi kinachoisimamia Serikali.

“Nimeshangazwa na hatua ya kuwazuia wabunge wasijadili mgomo wa madaktari kwa kigezo suala hili liko mahakamani, kesi iliyopo ni Serikali kukishtaki Chama cha Madaktari nchini (MAT).

“Mgomo uliopo sasa unasimamiwa na Jumuiya ya Madaktari nchini  ambayo haijashtakiwa mahakamani hivyo inashangaza Serikali kudai haiwezi kutoa kauli wakati kesi iko mahakamani,” alisema.

Aliongeza kuwa, jambo la kusikitisha wabunge wananyimwa ripoti ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Sekta ya Afya ambazo zilichunguza kiini cha mgogoro wa madaktari na Serikali.

Bw. Mnyika alisema, hivi sasa wanatarajia kuwasilisha malalamiko yao kwa Katibu wa Bunge kupinga maamuzi ya Spika kuzuia mjadala huo usiendelee bungeni kwani kanuni za Bunge la Jumuiya ya Madola ambazo ndio zinazotumika zinaelekeza hivyo.

Katika hatua nyingine, Mwandishi Stella Aron anaripoti kuwa, Jeshi la Polisi nchini, limewataka madaktari waliogoma kurudi kazini na kuheshimu viapo vyao kwani kuendelea na mgomo ni kuongeza vifo vya Watanzania wasio na hatia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Oparesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Bw. Paul Chagonja, alisema fani ya udaktari ni wito ambapo mahakama ilitoa uamuzi wa kusitisha mgomo huo.

“Mahakama ilishatoa amri ya kusitisha mgomo huu lakini bado madktari wameendelea kugoma, huu ni uvunjifu wa sheria za nchi hivyo tunawaomba watumie busara na kusitisha mgomo.

“Serikali imekuwa na uvumilivu mkubwa katika kutatua mgogoro uliopo ikitumia njia mbalimbali, sisi kama chombo cha dola tunaweza kumshtaki mtu asiyeheshimu sheria za nchi.

“Yeyote anayeonekana kutotii amri ya mahakama, tuna uwezo wa kumkamata na kumfungulia mashtaka,” alisema Kamanda Chagonjwa na kusisitiza kuwa, Jeshi la Polisi halihusiki na tukio la kumteka nyara Dkt. Steven Ulimboka.

Aliongeza kuwa, kama madaktari wameshindwa kukubaliana na amri hiyo wangetoa pingamizi katika mahakama ya rufaa ili sheria ichukue mkondo wake.

Alisema kitendo cha kukataa kutii sheria ni sawa na kufanya kosa hivyo si jambo la busara kuishinikiza Serikali ili ifanye jambo fulani badala ya kutumia njia za kidomokrasia.

Kamanda Chagonja alisema, jeshi hilo litaendelea kuwasaka watu waliohusika kumteka Dkt. Ulimboka ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Tume tuliyoiunda tutaendelea nayo, taaarifa za polisi kuhusika na tukio hili hazina ukweli, tunawataka madaktari warudi kazini vinginevyo sheria itachukua mkondo wake,” alisema.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limewakamata wahamiaji haramu 378 kutoka nchi zinazoinguka Tanzania wakiwa na silaha mbalimbali.

Kamanda Chagonja alisema, silaha zilizokamatwa ni short gun (5),   riffle (5), magobore (14), bastola (4), SMG (7) na risasi 123.

Alisema jeshi hilo pia limekamata dawa mbalimbali za kulevya ambazo ni heloin kilogramu 203, pombe haramu ya gongo lita 1,379, bangi kilo 239 na watuhumiwa 46.

2 comments:

  1. Tindu Lissu chama chako kinahusika na mchezo huo mchafu wa kutekwa nyara huyo daktari muuaji ili mnufaike kisiasa. ati unazungumzia atoke jaji atoke mahakama kuu na chama cha mawakili kitoe wawakilishi,naomba ujiulize mahakimu,majaji,mawakili na wewe ukiwa mmoja wapo mpo safi? nchi hii imekuwa balaa kabisa wasafi ni wachache sana na wachafu ndio wapigaji kelele wakubwa. nilitegemea Lissu utasema wanasiasa na vyama vyenu mnafilisi nchi kwa marupurupu na mishahara minono huku mkiwacha wataalamu wakiwa na mishahara midogo. Mhe. Rais madai ya madaktari kutaka mishahara na marupurupu makubwa ni kutokana na nyie wanasiasa kujipendelea kujipa mishahara na marupurupu manono, unategemea unaposema huna pesa za kuwalipa madaktari sisi tunauliza za kuwalipa wanasiasa na wabunge zinatoka wapi? mfagiaji wa BOT au TRA anapata mshahara mnono kuliko mtaalam,unategemea nini. NI MUHIMU KWAKO SASA KUFUTA RUZUKU ZA VYAMA VYA SIASA NA KUKATA NUSU YA MISHAHARA YA WABUNGE NA MAWAZIRI WAKO ILI UWEZE KUWALIPA MADAKTARI. SIKUBALIANI NA MARUPURUPU NA MISHAHARA YA DAKTARI ANAYEANZA KAZI ALIPWE Tsh 7,500,000/= MKAE MFIKIE MUAFAKA NA WEWE LISSU ,WANAHARAKATI NA WANASIASA ACHENI KULETA BLABLA KWENYE ISSUE NZITO KAMA HII MNAMZUNGUMZIA ULIMBOKA MMOJA KWA NGUVU YA ZIADA HUKU WENGINE WANAKUFA NA KUTESEKA MNAWAZUNGUMZIA KIUJANJAUJANJA TU.

    ReplyDelete
  2. sisi tunakufa wanasiasa hawazungumzii lakini kwa vile DR ULIMBOKA wanasiasa kama tundu lissu mlimtuma kuazisha mgomo ili wanachi tufe amepata janga hilo kila mtu anazungumzia hilo.VIPI HAPA TANZANIA KUNA WATETEZI WA HAZI ZA BINADAM, VIONGOZI WA DINI NA WANAHARAKATI MBONA WANAWANANCHI WANAKUFA WAO WAPO KIMYA? TUKISEMA WANAHUSIKA NA MGOMO WA MADAKTARI TUTAKOSEA.MIMI NAAMINI HATA WAO NI SEHEM YA WAMEHUSIKA NA MGOMO

    ReplyDelete