02 July 2012

Yanga kuanza na Atletico Kagame *Simba na wakusanya kodi wa Uganda URA



Na Elizabeth Mayemba

MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame Yanga wanatarajiwa kufungua dimba la michuano hiyo na timu ya Atletico ya Burundi, mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.

Wakati Yanga wakicheza Julai 14, mwaka huu mahasimu wao Simba wao watacheza Julai 16, dhidi ya URA ya Uganda katika uwanja huo huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Nicholaus Musonye, alisema siku ya ufunguzi mechi zitakazoanza saa nane mchana ni kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kaskazini.

Alisema katika Uwanja wa Azam uliopo Chamazi,Dar es Salaam Azam watacheza na Mafunzo ya Zanzibar, Julai 15,mwaka huu saa 10 jioni.

"Tunaimani mashindano haya yatakuwa bora zaidi kama ilivyokuwa mwaka jana, kulikuwa na upinzani mkubwa sana na mashindano yalipendeza," alisema Musonye.

Alisema kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), bado wanaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya michuano hiyo, hivyo milango ipo wazi kwa wadhamini ambao watataka kuwapa sapoti.

Katibu huyo alisema timu zinazoshiriki michuano hiyo zipo 11 na zimegawanywa katika makundi matatu, ambapo kundi A lina timu za Simba, URA ya Uganda, Vita ya Kongo na Ports ya Djbout.

Kundi B kuna timu za Azam FC, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya na kundi C kuna Yanga, APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kaskazini na Atletico ya Burundi.

Musonye alisema zawadi kwa mshindi wa kwanza ni kombe na dola 30,000, wa pili dola 20,000 na watatu dola 10,000.

No comments:

Post a Comment