02 July 2012
Simba kwenda Z'bar kupiga kambi
Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara Simba, wanatarajiwa kwenda visiwani Zanzibar keshokutwa kupiga kambi kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame.
Michuano hiyo imepangwa kuanza Julai 14, mwaka huu Dar es Salaam ambapo Simba imepangwa Kundi A ikiwa na timu za URA ya Uganda, Vita Club ya Congo DR na Ports ya Djibouti.
Simba imepangwa kucheza Julai 16 na URA katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema timu hiyo itapiga kambi visiwani humo mpaka siku moja kabla ya michuano hiyo kuanza.
Alisema timu yao kwa sasa inaendelea na mazoezi kwenye viwanja vya TCC, Sigara chini ya kocha wao, Milovan Cirkovic ambapo kikubwa wanachokifanya kwa sasa ni kuuchezea mpira muda mwingi.
"Milovan ameomba timu hiyo iweke kambi visiwani humo ili iwe na stamina ya kutosha na pia watashiriki katika michuano ya Ufariki iliyopangwa kufanyika visiwani humo," alisema Kaburu.
Alisema kabla hawajaondoka wanafanya mpango kesho timu hiyo icheze mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya The Express ya Uganda ambayo walishacheza nayo hivi karibuni Kanda ya Ziwa na kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Alisema mechi hiyo ni maalum kwa ajili ya Milovan kuangalia wachezaji wake wapya ambao wamesajiliwa hivi karibuni na pia atawaangalia katika michuano ya Urafiki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment