10 July 2012

Yanga kuanika vifaa vyao leo



Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, timu ya Yanga, leo inaanika 'vifaa' vyao vipya vitakavyowatumia katika kombe hilo na Ligi Kuu Bara wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu, itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Katika mechi hiyo, viingilio ni sh. 3,000 kwa viti vya kijani, sh. 5,000 kwa viti vya machungwa, Viti Maalum (VIP) B na C ni sh. 10,000 na VIP A ni sh. 15,000.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa mechi hiyo, Salim Mkemi alisema wameamua kuandaa mechi hiyo ili kuiandaa Yanga kwa ajili ya kutetea kombe hilo.

"Lengo kubwa ni kuhakikisha kombe hilo linabaki hapa nyumbani, hivyo baada ya kukubaliana na uongozi wa Yanga, tukaona tuitafutie timu hiyo ili ijipime pamoja na kuwaangalia wachezaji wao wapya," alisema Mkemi.

Naye Ofisa Habari wa timu ya Yanga, Louis Sendeu alisema mechi hiyo ni kipimo kizuri kwao kwani JKT ni moja kati ya timu zinazotoa ushindani katika ligi kuu, hivyo ana uhakika ni kipimo kizuri.

Alisema mechi hiyo ni maalum kwa ajili ya kuweka hadharani kikosi chao kipya kitakachoshiriki kombe hilo pamoja na ligi kuu, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi.

"Kesho (leo) tutafanya suprise kwa mashabiki wetu kwani kuna nafasi mbili za kimataifa zilizoachwa na Kenneth Asamoah na Davis Mwape hazijazibwa, hivyo watakaokuja uwanjani watajua nafasi zao zimezibwa na akina nani," alitamba Sendeu.

Alisema mchezo huo pia utakuwa ni fursa nzuri kwa Kocha Mkuu, Mbelgiji, Tom Seintfeit kuona aina ya wachezaji alionao pamoja na kupata kikosi cha kwanza.

Mchezo huo wa kirafiki ni wa pili kwa Yanga ambapo awali walicheza na The Express ya Uganda na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment