10 July 2012

Milovan: Simba imeiva Kagame



Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Simba Milovan Cirkovic amesema kwamba michuano ya Urafiki Tanzania inayoendelea visiwani Zanzibar kwa kiasi kikubwa imemsaidia kupata kikosi cha kwanza kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Kagame, inayoanza kutmua vumbi Julai 14, mwaka huu.


Katika michuano ya Kagame Simba wataanza kibarua chao Julai 16, mwaka huu ambapo watavaana na URA ya Uganda, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.

Akizungumza kutoka visiwani Zanzibar jana, Milovan alisema kwa sasa kikosi chake kina wachezaji wengi wapya hivyo michuano ya Urafiki kwa kiasi kikubwa imewafanya wachezaji wake wazoeane.

"Nimefurahi sana kupata michuano hii kwani ilikuwa ngumu sana wachezaji wangu kuzoeana, lakini kwa sasa wanaendelea vizuri na wananipa matumaini makubwa katika michuano ijayo," alisema Milovan

Kocha huyo raia wa Serbia alisema bado anaendelea kufanyia kazi zaidi kikosi chake katika safu  ya ushambuliaji, kwani kiungo na beki haina tatizo kama ni matatizo basi madogo madogo ya kiufundi.

Milovan alisema hata hivyo anaridhishwa na kiwango kinachooneshwa na wachezaji wake katika michuano hiyo, na pia kumekuwa na ushindani mkubwa sana wa namba katika kikosi chake huku kila mmoja akitaka kujihakikishia namba katika kikosi cha kwanza.

"Idara moja ikiwa na wachezaji wengi ni nzuri sana kwani kila mmoja atakuwa akionesha uwezo binafsi ili apete namba, hali ambayo itachangia kuwa na wachezaji wengi wazuri bila kumtegemea mchezaji mmoja mmoja," alisema

Jana jioni timu hiyo ilitarajiwa kushuka uwanjani kucheza na Zanzibar All Stars katika nusu fainali ya michuano ya Urafiki Tanzania.

No comments:

Post a Comment