16 July 2012

Yanga, Atletico kazi ipo leo Kagame *TBL 'yazipiga pamba' Simba, Yanga



Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, timu ya Yanga, leo itashuka uwanjani kutetea ubingwa wake kwa kuumana na Atletico ya Burundi katika mechi itakayopigwa saa 10 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Kabla ya mechi hiyo kuchezwa, itatanguliwa na mchezo kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya Sudan kwenye uwanja huo huo.

Yanga itashuka uwanjani ikiwa na nahodha mpya, Nadir Haroub 'Canavaro' akisaidiana na Athuman Idd 'Chuji' baada ya aliyekuwa nahodha, Shadrack Nsajigwa kutemwa.

Wachezaji wapya wa timu hiyo, Said Bahanuzi, Nizar Khalfan, Kelvin Yondani, Ally Mustapha 'Barthez', Juma Abdul na Ladslaus Mbogo watakuwa na kazi ya ziada ya kuonesha thamani yao kwa kuhakikisha kombe hilo linabaki Jangwani.

Si kwa wachezaji hao wapya tu, hata kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfeit ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili, atakuwa na kibarua cha kuendelea kuweka matumaini kwa wanachamana wapenzi wa timu hiyo kama walivyoweka wakati alipotua nchini.

Akizungumzia mashindano hayo juzi, Saintfeit alisema ana kikosi bora lakini amechagua 20 watakaowawakilisha wengine huku akisikitishwa kukosekana kwa nyota Simon Msuva, Frank Damayo na Omega Seme.

Yanga ilitwaa ubingwa huo baada ya kuichapa Simba bao 1-0 lililofungwa dakika ya 110 kupitia kwa Keneth Asamaoh, aliyeingia kuchukua nafasi  ya Jerry Tegete kwa kichwa akiunganisha krosi kutoka wingi ya kushoto.

Katika hatua nyingine, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Lager, imetoa vifaa vya michezo kwa ajili ya michuano hiyo kwa Yanga na Simba vyenye thamani ya sh. milioni 70.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo Dar es Salaam jana, Kaimu Meneja wa bia ya Kilimanjaro, Oscar Shelukindo alisema kufanya hivyo ni kutimiza moja ya masharti ya mkataba walioingia na klabu hizo.

Alisema ana imani vifaa hivyo vitachangia kwa kiasi kikubwa timu hizo kupigana kufa au kupona kuhakikisha kombe hilo linabaki nchini kwa mara nyingine.

Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' aliishukuru kampuni hiyo kwa kuendelea kutimiza moja ya makubaliano yao na kwamba watajitahidi kulibakisha kombe nchini.

Naye Mwakilishi kutoka Yanga, Hafidh pia aliishukuru kampuni hiyo na kuwaahidi mashabiki wa timu hiyo watahakikisha watetea ubingwa walioutwaa mwaka jana.

No comments:

Post a Comment