16 July 2012
Dkt. Slaa apinga madai ya mkewe *Awasilisha pingamizi Mahakama Kuu Dar *Mawakili wavutana, kusikilizwa Agosti 14
Na Rehema Mohamed
SIKU moja baada ya Bi. Rose Slaa ambaye ni mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, kufungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ili kupinga ndoa ya mumuwe na Bi. Josephine Mshumbusi, Katibu Mkuu huyo naye amewasilisha pingamizi la kupinga hati hiyo ya madai.
Pingamizi hilo limewasilishwa mahakamani hapo jana na Bw. Mutakyamirwa Philemon ambaye ni Wakili wa Dkt. Slaa, mbele ya Jaji Raulence Kaduri, wakati kesi hiyo ilipoletwa kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu wa Bw. Philemon, katika pingamizi hilo wanapinga hati ya madai ya Bi. Slaa na kudai kuwa, kesi zinazohusiana na ndoa hazipaswi kupelekwa mahakamani kama hati ya madai inavyosema isipokuwa kwa kiapo au maombi.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Kaduri alipanga pingamizi hilo kuanza kusikilizwa Agosti 14 mwaka huu.
Wakati huo huo Jaji Kaduri alimtaka Bw. Philemon, kujibu hati ya madai ya Bi. Slaa kwa njia ya maandishi kabla ya Julai 30 mwaka huu. Pia alimtaka Bw. Joseph Tadayo ambaye ni Wakili wa Bi. Slaa, kuwasilisha hoja za nyongeza Agosti 7 mwaka huu.
Bi. Slaa amefungua kesi ya masuala ya ndoa namba 4/2012 mahakamani hapo Julai 5 mwaka huu, dhidi ya Dkt. Slaa na mchumba wa Bi. Mshumbusi.
Katika kesi hiyo, Bi. Slaa anaiomba mahakama imtanganze yeye na Dkt. Slaa, kuwa bado ni wanandoa halali kisheria ambapo ndoa nyingine ambayo itafungwa itakuwa batili.
Pia anaiomba mahakama hiyo iwaamuru wadaiwa katika shauri hilo wamlipe fidia ya sh. milioni 50 kama gharama za matunzo ya watoto watoto wawili aliozaa na Dkt. Slaa.
Bi. Slaa pia ameiomba mahakama imwamuru Bi. Mushumbusi amlipe fidia ya sh. milioni 500 kwa sababu alimsababishia usumbufu mkubwa na kumharibia ndoa yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment