16 July 2012

Kampeni chafu zatawala Yanga *Ni kuelekea uchaguzi wa viongozi wake


Na Eliabeth Mayemba

KAMATI ya Uchauzi ya Yanga imelaani kampeni chafu zinazofanywa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, ambapo wameahidi kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaobainika.

Uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika kesho katika ukumbi wa Diamond Jubilee,Dar es Salaam ambapo uhakiki kwa wanachama wote utaanza saa 12 asubuhi na zoezi la kupiga kura ni saa sita mchana.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, Francis Kaswahili alisema kuna kampeni chafu ambazo zimejitokeza kwa baadhi ya wagombea kuchapisgha majina ya wagombea sita na kuwataka wanachana wawapigie kura.

"Tutachunguza kwa umakini mkubwa kwa atakayebainika tutamchukulia hatua kali za kinidhamu na kama kutakuwa na mgombea anayehusika kwa hili naye tutamuondoa kwenye kinyang'anyiro endapo atabainika," alisema Kaswahili.

Alisema kamati inaziita kampeni hizo kuwa ni chafu kwani kila mwanachama ana haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka na sikulazimishwa.

Katika hatua nyingine Kaswahili ametoa karipio kali kwa mwanachama yeyote ambaye atakwenda mahakamani kuzuia uchaguzi huo, kwani mtu huyo haitakii mema klabu.

"Kikubwa tunachotaka ni kupata viongozi, sasa kuna vitisho ambavyo vimeanza kujitokeza kwa baadhi ya wanachama kutaka kusimamisha uchaguzi, kamati inachunguza na itachukua hatua kali kwa atakayebainika," alisema.

Alisema kwanza kabisa watamshitaki mtu huyo, pia atapelekwa katika Kamati ya nidhamu ya Yanga kwa ajili ya kutolewa maamuzi ikiwa na kufutwa uanachama wake.

No comments:

Post a Comment