31 July 2012

Watumishi Pori la Akiba wadaiwa kuchoma moto bendera ya CCM


Na Said Njuki, aliyekuwa Kondoa

MGOGORO uliodumu muda mrefu kati ya wakazi wa Vijiji vya Ikengwa, Keikei na Idindiri, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma na watumishi wa pori la Akiba la Mkungunero, lililopo katika vijiji hivyo, umechukua sura mpya.

Hali hiyo inatokana maofisa wa pori hilo, kudaiwa kuchoma bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kushinikiza wananchi hao kuondoka katika maeneo hayo.

Mbali na madai ya kuchomwa moto kwa bendera hiyo, watumishi hao pia wanadaiwa kunyanyasa wananchi kwa kuwapiga bakora bila kujali umri wa mtu na kuwataka waondoke kwenye mashamba ambayo wananchi walikuwa wakiyalima muda mrefu.

Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakulima wa eneo la Ngurutu, walidai manyanyaso wanayofanyiwa na maofisa hao yanaweza kupoteza amani iliyopo hivyo kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi kuingilia kati.

“Hawa watumishi walifika nyumbani kwangu eneo la Ngurutu, Kata ya Itaswi, Julai 14 mwaka huu wakiwa na gari aina ya Land Rover STK 110, wakati huo mimi nilikuwa shambani.

“Walipofika walimkuta mke wangu na mama wa jirani, waliwatishia maisha na kuteremsha bendera ya CCM iliyokuwa katika tawi letu na kuichoma moto wakidai eneo hilo si la kuweka bendera ya chama, mimi sikatae ila kwanini wameichoma,” alihoji Bw. Haji Shaaban ambaye ni mkulima wa eneo hilo.

Mkulima mwingine Bw. Adamu Mmasy, alisema mbali ya vitisho wanavyopewa na watumishi hao, pia wamekuwa wakitumia bakora kuwapiga wananchi ili kushinikiza waondoke na kudai wanyama kama dikidiki wana thamani kubwa kuliko binadamu.

“Mzee Mohamed Mcholo alicharazwa viboko na hawa watumishi, aliuguza majeraha yake bila kujua ni wapi atapeleka malalamiko yake,” alisema Bw. Mmasy.

Diwani wa kata hiyo, Bw. Said Chobu, alikiri kuwepo tatizo hilo na kudai kuwa, yeye mwenyewe ana shamba la zaidi ya ekari 300 katika eneo hilo lakini amelazimika kukimbiza maisha yake akihofia kipigo kutoka kwa watumishi hao.

Meneja wa pori hilo Bw. Ernest Madanya, alikiri kufika nyumbani kwa Bw. Shaaban na kuwakuta akina mama hao pamoja na wenzake lakini alikataa kuhusika na ushushaji bendera ya CCM, kuichoma moto na kusisitiza wakulima hao wanaishi kinyume cha sheria.

Alesema eneo hilo ni tengefu hivyo hakuna sababu ya wakulima hao kuling'ang'ania bali wanapaswa kuondoka ili kumpisha mwekezaji ambaye anafanya kazi ya uwindaji wa kitalii ambayo haiwezi kuchanganya na shughuli za kilimo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya humo, Bw. Athumani Gora, alikiri kusikia madai ya bendera ya chama kuchomwa moto na kuahidi kufuatilia sakata hilo kwani kitendo hicho si cha kiungwana.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Omari Kwaang’, alisema licha ya ugeni wake wilayani humo, tayari amepata taarifa juu ya mgogoro huo hivyo ataushughulikia kwani wakati huu si malumbano.


No comments:

Post a Comment