31 July 2012

Gari la kanisa laua watoto wawili, wanakwaya sita



Na Bryceson Mathias, Mvomero

GARI la Parokia ya Mt. Theresia Maskati, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, limepinduka na kuua wanakwaya sita, watoto wawili papo hapo na kujeruhi wengine 13 wakati wakienda kutoa huduma ya ekaristi na ubatizo kwenye Kigango cha Chaginali.

Ajali hiyo ilitokea Julai 28 mwaka huu ambapo gari hiyo aina ya Niva ilikuwa na namba za usajili T 575 AHY.

Majira lilizungumza na majeruhi wa ajali hiyo katika Hospitali ya Misheni Bwagala, ambao walisema dereva wao Padri Baharia Maliwa, alikuwa katika mwendo wa kawaida ila chanzo cha ajali ni kufeli kwa breki walipofika kwenye kona.

Waliokufa katika ajali hiyo Godfrey Kisonye, Frorence Luka,  Secilia Isaya, Theodosia Jeremia, Leti Kiondo, Betina Jakobo, watoto Lily Jakobo na Elizabeth Karoli.

Majeruhi Bw. Frank Posian, Bw. Antony Joseph na Bw. Indesi Jeremia ambao walizungumza na gazeti hili, walisema breki hizo zilifeli katika kona ya Mkondeni karibu na kibaoni.

Bw. Peter Mnugu ambaye amekatika vidole viwili vya mkono wa kushoto, alidai kusikia maumivu makali na hakuwa tayari kuzungumzia mazingira ya ajali hiyo.

Bi. Hilder Frolian aliyelazwa wodi ya wanawake, naye alishindwa kuzungumzia ajali hiyo kwa sababu muda huo alikuwa akitoka katika chumba cha upasuaji ila mama yake Bi. Froliani, alisema
mwanaye ameumia sana ndani ya mwili.

Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani hapa, Bw. Hamisi Selemani, alithibitisha kutokea ajali na vifo hivyo.


No comments:

Post a Comment