31 July 2012

Sabodo: Wanaotaka kuchimbiwa visima vya maji leteni maombi



Na Mwandishi Wetu

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mfanyabiashara maarufu nchini, Bw. Mustafa Sabodo, amewata wananchi na taasisi mbalimbali zikiwemo za dini ambazo zinahitaji msaada wa kuchimbiwa visima vya maji, wampelekee maombi.


Bw. Sabodo aliyasema hayo Dar es Salaam juzi baada ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philipo Mulugo kumtembelea nyumbani ili kumshukuru kwa msaada aliompa wa kumchimbia visima 17 katika Jimbo lake la Songwe, mkoani Mbeya ambavyo vimegharimu sh. milioni 300.

Alisema misaada ya uchimbaji visima anayotoa kwa viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge, haiangalii itikadi za kisiasa bali dhamira yake ni kusaidia wananchi.

“Misaada ninayotoa siangalii itikadi za vyama bali dhamira yangu ni kusaidia wananchi ambao ndio wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha,” alisema Bw. Sabodo.

Alisema yupo tayari kutoa misaada zaidi katika jimbo hilo na kusisitiza kuwa, misaada anayotoa haibagui chama chochote cha siasa ambapo hivi sasa anajenga jengo la ghorofa ambalo litatumika kwa maegesho ya magari.

“Fedha ambazo zitapatikana katika maegesho haya kwa kipindi cha miaka 10, zitatumika kuchimba visima kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema Bw. Sabodo.

Kwa upande wake, Bw. Mulugo alisema visima hivyo vitasaidia kuondoa kero ya maji jimboni kwake na kumkabidhi Bw. Sabodo, zawadi ya picha ya sanamu inayoonesha ramani ya Afrika pamoja na picha ya mfano wa visima.

Alisema picha ya sanamu imelenga kutambua mchango wa Bw. Sabodo si kwa Tanzania bali kwa bara zima la Afrika ambapo ile ya visima ni kumbukumbu ya misaada anayotoa kwa kuchimba visima katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika hafla ya uzinduzi wa visima hivyo, Bw. Mulugo aliwataka wananchi kuvitunza vizuri badala ya kuwaacha watoto waende kuchota maji na kuchezea pampu ambazo zinaweza kuharibika.

Aliuagiza uongozi wa vijiji kutafuta vijana waliohitimu mafunzo ya mgambo na kuwaajiri ili kulinda visima hivyo visiweze kuhujumiwa na watu wasiopenda maendeleo.

“Nipo tayari kulipa mshahara wa sh. 50,000 kwa kila mlinzi mmoja katika visima hivi pamoja na kugharamia chakula,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bw. Maurice Sapanjo, alisema pamoja na mradi huo kuwa wa mbunge, hivi sasa ni mali ya umma hivyo unapaswa kutunzwa na kuheshimiwa.

“Serikali za vijiji zinapaswa kuhakikisha visima hivi vinakuwa salama na kutumika muda wote ili wananchi wasipate shida ya maji kama ilivyokuwa zamani ambapo hadi sasa, visima 10 ndio vimekamilika na kazi ya uchimbaji vingine inaendelea.

2 comments:

  1. Sasa mbona hamjaweka mawasiliano ya Sabodo? au nitampata vipi naomba msaada wa kumpata. Naomba mnijulishe kwa anuanuni hii vonostust@gmail.com

    ReplyDelete
  2. Rev Josephat KaboyaAugust 2, 2012 at 4:52 PM

    Jamani hata mimi nahitaji msaada wa mzee sabodo,nahitaji kwenda soma nchi za nje lakini mpaka sasa sijapata mwelekeo wowote na muda nao ndo unazidi yoyoma,kwani chuo kitafunguliwa mwezi sptemba mwaka huu (yaani 2012) nipeni mawasiliano yake kupitia e-mail address ifuatayo: revjskaboya@yahoo.com

    ReplyDelete